NEWS

Friday 18 September 2020

CRDB Tarime yawapa Vicoba elimu ya mikopo

Meneja Biashara wa Benki ya CRDB Tawi la Tarime, Mahadi Mkungile akizungumza na wajasiriamali wa Vicoba wilayani humo katika semina iliyoandaliwa na benki hiyo kuwajemngea uwezo wa kukopa na kukuza biashara zao.

 

BENKI ya CRDB Tawi la Tarime leo Septemba 18, 2020 imewakutanisha wajasiriamali wa Vicoba zaidi ya 200 kutoka wilayani hapa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kukopa fedha kwa masharti nafuu ili kukuza mitaji ya biashara zao.

 

Akitoa semina hiyo kwa wajasiriamali hao katika ukumbi wa Blue Sky mjini Tarime, Meneja Biashara wa Benki ya CRDB Tawi la Tarime, Mahadi Mkungile amesema elimu hiyo inalenga kuhamasisha ufunguzi wa akaundi za Vicoba na za mjasiriamali mmoja mmoja katika shughuli zao za kibiashara.

Baadhi ya wajasiriamali wa Vicoba wilayani Tarime wakiwa katika semina iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kuwajengea uwezo namna ya kukopa na kukuza biashara zao.


Mkungile amesema benki hiyo inatoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo ambapo imepunguza riba kutoka asilimia 20 hadi 14 kwa wanawake na pia amewakumbusha kutumia huduma za bima zikiwemo za gari, pikipiki, nyumba, biashara na afya.

 

Pia amewakumbusha wajasiriamali kuendelea kutumia huduma mbadala zikiwemo huduma za wakala zinazopatikana sehemu mbalimbali na kujiunga huduma za simbanking ili kurahisisha ufanyikaji wa miamala. 

 

Meneja huyo ameongeza kuwa Benki ya CRDB inatoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja kwa masharti nafuu na kurahisisha kigezo cha dhamana ikiwemo matumizi ya barua ya mauziano au hati ya kimila kwa ajili ya dhama ya mkopo.

Mwenyeki na mlezi wa vikundi Vicoba Wilaya ya Tarime, Daniel Cheo (kushoto) akizungumza katika semina iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kuwajengea uwezo wa kukopa na kukuza biashara zao. Katikati ni Meneja Biashara wa benki hiyo tawi la Tarime, Mahadi Mkungile.


 

Mkungile pia amewahamasisha wajasiriamali hao kujitokeza kutumia fursa hiyo ili kuendeleza biashara zao.

 

Katika semina hiyo, wajasiriamali hao wamepewa fursa ya kuuliza na kujibiwa maswali kuhusu huduma na bidhaa zinazotolewa na Benki ya CRDB.

 

Mwenyekiti na mlezi wa vikundi vya ujasiriamali Wilaya ya Tarime, Daniel Cheo ameishukuru Benki ya CRDB kwa semina hiyo na kuahidi kuendelea kuitumia katika kukuza biashara zao.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages