NEWS

Friday 18 September 2020

Majaliwa: CCM ni baba lao

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto) na mgombea ubunge jimbo la Bariadi kwa tiketi ya CCM, Mhandisi Kundo Andrea Mathew (kulia) wakizungumza katika mkutano wa kampeni Bariadi, juzi.

 

WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NCE) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, chama hicho kimeweza kuwaletea wananchi maendeleo makubwa katika sekta zote, hivyo wananchi waendelee kukiamini kwa kukipigia tena kura ili wafanye zaidi ya walipofanya.

 

Mbali na hilo, amewaomba wananchi wa mkoa wa Simiyu na wanachama wa vyama vingine vya upinzani kutoogopa kuwapigia kura wagombea wa CCM kwani ndicho chama pekee kilicho imara na kinachotekeleza ilani yake kwa vitendo.

Majaliwa ameyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa jimbo la Bariadi, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nkololo wilayani Bariadi, Simiyu.

Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani) katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge jimbo la Bariadi, juzi."Wananchi wote wa mkoani hapa (Simiyu) bila kujali vyama vyenu siku ya kupiga kura wachagueni wagombea wa Chama Cha Mapinduzi na epukeni kuchanganya viongozi wa CCM na vyama vingine kwani kwa kufanya hivyo watashindwa kuwa kitu kimoja wakati wa utekelezaji wa ilani ya chama,” amesema Majaliwa na kuongeza:

"Chama Cha Mapinduzi kina benki ya viongozi wa kutosha ambao wanaweza kufanya kazi ipasavyo kwa kuzingatia ilani ya chama, hivyo ni vema mkatumia haki yenu ya msingi na ya kikatiba kwa kuchagua viongozi bora watakaotatua kero na changamoto za wananchi.”

Baadhi ya makada wa CCM waliojitokeza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge jimbo la Bariadi uliohutubiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, juzi.


Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Bariadi, Mhandisi Mathew, amewaomba wakazi wa jimbo hilo kumchagua ili aweze kushirikiana na serikali katika  kutatua changamoto mbalimbali na kuleta maendeleo jimboni.

"Natambua kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na watangulizi wangu ndani ya jimbo la Bariadi ila nami niwahakikishie wananchi ushirikiano wa karibu katika kuendeleza miradi iliyoachwa na mtangulizi wangu, Andrew Chenge, nichagueni nikawatumikie," amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia mikono wakazi wa Bariadi alipokwenda kuzindua kampeni za mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, juzi.


Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Enock Yakobo amewataka wagombea wote wa chama hicho pindi watakapochaguliwa kuhakikisha wanatimiza ahadi zao ili chama hicho kizidi kuaminiwa kama ambavyo kimeendelea kuaminiwa kwa utekelezaji wa ahadi zake kwa wakati.


(Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages