WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewaomba wakazi wa jimbo la Tarime Vijijini kuhakikisha wanamchagua mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara, akisema ndiye suluhisho thabiti la matatizo yanayowanyima maendeleo ya kweli.
“Waitara ni kijana mchapa kazi, ameweza kufanya mambo mengi kwa maendeleo ya wananchi kupitia nafasi ya naibu waziri [wa Tamisemi], mchague huyu atakuwa msaada mkubwa kwenu wana-Tarime Vijijini.
“Mchagueni Waitara maana ana uwezo wa kuingia kwa rais moja kwa moja bila hodi, ataingia kwangu [Waziri Mkuu] na kwa waziri yeyote bila hodi kuwasilisha changamoto zenu na kuwaombea miradi ya maendeleo,” amesisitiza Majaliwa aliposimama barabarani kuzungumza na wananchi eneo la Nyamongo na baadaye Nyamwaga na mjini Tarime, leo Septemba 20, 2020.
Majaliwa amefafanua kuwa wakazi wa jimbo la Tarime Vijijini wakimchagua Waitara atashirikiana na Rais na yeye mwenyewe (Waziri Mkuu) kuharakisha ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili yakiwamo ya malipo ya fidia kwa waliohamishwa kupisha mgodi wa dhahabu wa North Mara na upatikanaji wa ajira za wazawa katika mgodi huo.
Pia Waiatala atasaidia upatikanaji wa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria, kupandisha hadhi eneo la Nyamongo kuwa mamlaka ya mji, ujenzi wa barabara ya lami ya Tarime – Nyamwaga hadi wilayani Serengeti, kurejesha mpango wa mgodi kugharimia mahitaji ya wanafunzi wa sekondari na vyuo, kuboresha huduma za afya na elimu, miongoni mwa huduma nyingine za kijamii na kiuchumi.
Waziri Mkuu ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba wakazi wa jimbo la Tarime Vijijini kumchagua mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt John Pombe Magufuli na wagombea udiwani katika kata mbalimbali jimboni humo wanaotokana na chama hicho.
Amefafanua kuhusu umuhimu wa kuchagua rais, wabunge na madiwani wanaotokana na CCM kuwa ni kuunda jopo la viongozi watakaozungumza lugha moja inayolenga kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Naye Waitara ameahidi akipewa ridhaa ya kuwa mbunge wangusha wananchi wa jimbo la Tarime Vijijini akisema atatumia muda mwingi kuwasumbua Rais, Waziri Mkuu na viongozi wa wizara mbalimbali kwa ajili ya kuwaletea maendeleo ya kisekta.
(Habari na picha zote na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment