HALMASHAURI ya Mji wa Tarime mkoani Mara juzi Oktoba 15, 2020 imezindua Baraza la Wazee litakalokuwa mhimili wa kutetea masuala ya kundi hilo la jamii katika halmashauri hiyo.
Hatua hiyo imefikiwa kutokana na msukumo wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Elias Ntiruhungwa ambaye anakazania mpango wa kuhakikisha wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wanapata vitambulisho vitakavyowawezesha kupata matibabu bila malipo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa. |
Tayari Mkurugenzi Ntiruhungwa ameshafanikisha utengenezaji wa vitambulisho vya matibabu kwa wazee wa kata zote nane zinazounda Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa baraza hilo, Afisa Tarafa ya Inchage, Jonathan Machango aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri kwa nafasi ya mgeni rasmi, amepongeza hatua hiyo akisema ni kielelezo cha kuwatambua na kuwathamini wazee kama rasilimali na hazina muhimu katika maendeleo ya Taifa na jamii nzima.
Afisa Tarafa ya Inchage, Jonathan Machango aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Tarime, akizungumza katika hafla hiyo, juzi. Aliyekaa ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Dkt Calvin Mwasha. |
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirika lisilo la Kiserikali la Wazee wa Tarime (Saved Aged People in Tarime – SAPITA), Simon Chacha ameishukuru serikali kwa kukubali kuwa nao katika hafla ya uzinduzi wa baraza lao uliofanyika sambamba na ugawaji wa vitambulisho vya matibabu bila malipo kwa wazee wa Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Dkt Calvin Mwasha amesema serikali inatambua uwepo na umuhimu wa wazee, hivyo imeamua kuwapatia vitambulisho hivyo ili kuwarahisishia kupata huduma za afya bila malipo kwa wepesi zaidi.
“Dawa ambazo mlikuwa mnazikosa sasa zinapatikana kwa ajili yenu kwa hiyo ukiwa na kitambulisho hiki kitakuwezesha kupata huduma za afya bure, hivyo familia na wazee tuwajibike kuwatunza wazee,” amesema Dkt Mwasha.
Dkt Mwasha ameongeza kuwa lengo la maadhimisho ya siku ya wazee na uzinduzi wa baraza hilo ni kujenga jamii yenye kutambua na kulinda haki za msingi za wazee katika jamii.
Mratibu wa Lishe katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, Monica Ouko amewakumbusha wazee kuzingatia ulaji wa vyakula vyenye lishe na kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao.
Mratibu wa Lishe katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, Monica Ouko akizungumza katika hafla hiyo, juzi. |
Akizungumza kwa niaba ya wazee, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Joseph Nyiraha amemshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Ntiruhungwa, kufanikisha mpango wa kuwapatia vitambulisho vya matibabu bila malipo na kuahidi kuendelea kuisaidia serikali katika ulinzi wa amani na kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani.
Viongozi wa Baraza la Wazee katika picha ya pamoja na viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Mji wa Tarime wakati wa uzinduzi wa baraza hilo mjimni Tarime, juzi. (Picha zote na Peter Hezron) |
Maadhimisho hayo yamefanyika sambamba na kaulimbiu inayosema “2020 uchaguzi wa mwaka huu uwe wa amani na upendo”.
(Imeandikwa na Lilian Tesha, Tarime)
No comments:
Post a Comment