NEWS

Sunday 25 October 2020

Msimamizi Uchaguzi Tarime Mjini awataka wasimamizi wa vituo kutoa huduma bila upendeleo

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tarime Mjini, Elias Ntiruhungwa akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura jimboni humo, leo asubuhi.

 

MSIMAMIZI wa Uchaguzi Jimbo la Tarime Mjini, Elias Ntiruhungwa amewataka wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kutoa huduma zisizo na upendeleo wowote siku ya uchaguzi mkuu.

 

Ntiruhungwa amesisitiza hayo leo Oktoba 25, 2020 mjini Tarime wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura jimboni humo kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao siku ya uchaguzi.

Sehemu ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura jimbo la Tarime Mjini wakifuatilia mada katika mafunzo ya siku mbili ya kuwajegea uwezo yaliyoanza leo kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Tarime (TTC).

 

“Mmeaminiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), na ninyi mwaminike, siku ya uchaguzi mtoe huduma zisizo na upendeleo wowote, msikiuke sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi,” Ntiruhungwa amewambia wasimamizi hao.

 

Aidha, amewataka wasimamizi hao kutambua kuwa uchaguzi mkuu uko mikononi mwao, hivyo wana jukumu la kuhakikisha taratibu za NEC zinazinafuatwa kikamilifu ili kuepusha malalamiko na vurugu wakati wa kupiga kura na kutangaza matokeo.

Baadhi wasimamizi wa vituo vya kupigia kura jimbo la Tarime Mjini wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo kwenye ukumbi wa TTC mjini Tarime leo.

 

“Nini wasimamizi wa vituo vya kupigia kura ndio wenye uchaguzi, ninyi ndio mnatakiwa kuwa makini kuliko mtu mwingine yeyote kutokana na majukumu mliyonayo vituoni,” amesisitiza msimamizi huyo wa uchaguzi jimbo la Tarime Mjini.

 

Pia Ntiruhungwa amewataka wasimamizi hao kuhakikisha kila mmoja simu yake inakuwa hewani kipindi chote cha upigaji kura na utangazaji matokeo ya uchaguzi kwa ajili ya mawasiliano na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo na wasaidizi wake wakati wowote ikihitajika.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tarime Mjini, Elias Ntiruhungwa akiapisha wasimamizi wa vituo vya kura jimboni humo kabla ya kuanza mafunzo ya kuwajengea uwezo leo asubuhi kwenye ukumbi wa TTC.


Awali, kabla ya kuanza mafunzo hayo, wasimamizi hao wa vituo wamekula viapo viwili mbele ya Ntiruhungwa; cha kujitoa kwenye uanachama wa vyama vya siasa na cha kutunza siri za uchaguzi mkuu vituoni.

Baadhi ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura jimbo la Tarime Mjini wakila viapo vya kujiondoa kwenye uanachama wa vyama vya siasa na kutunza siri za uchaguzi, leo asubuhi kwenye ukumbi wa TTC.


“Suala la kutunza siri za uchaguzi ni la kisheria, hivyo ukitoa siri ya uchaguzi nje ya chumba cha kupigia kura utachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kushitakiwa mahakamani,” amesema Ntiruhungwa.

 

Mafunzo na viapo hivyo vimewashirikisha wasimamizi 575 wa vituo 181 vya kupigia kura katika jimbo la Tarime Mjini kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 28, 2020.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages