NEWS

Thursday, 10 July 2025

Wanafunzi 2,891 Mara wang’ara Mtihani wa Kidato cha Sita 2025, Mkuu wa Mkoa awapa kongole



Mkuu wa Mkoa wa Mara, 
Kanali Evans Alfred Mtambi.
-----------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, amewapongeza wanafunzi 2,891 katika mkoa huo waliopata ufaulu wa daraja la kwanza katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita kwa mwaka 2025.

Kanali Mtambi alitoa pongezi hizo juzi ofisini kwake mjini Musoma, baada ya kupokea taarifa za elimu zinazoonesha kuwa wanafunzi 2,891 sawa na asilimia 61.4 ya wanafunzi 4,708 wa mkoani Mara waliofanya mtihani huo wamepata ufaulu wa daraja la kwanza.

Aidha, aliwapongeza walimu kwa kazi nzuri iliyowezesha kupata matokeo mazuri, ambapo wanafaunzi waliopata daraja la pili ni 1,597 sawa na asilimia 33.9, huku waliopata daraja la tatu wakiwa 220 sawa na asilimia 4.67 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo.

“Ninapongeza sana kwa matokeo haya, shule zimejitahidi sana kuwasimamia wanafunzi vizuri na wote wamefaulu vizuri, hongereni sana,” alisema.

Alitumia nafasi hiyo pia kuitaka idara ya elimu katika mkoa huo kuandaa kikao cha tathmini kitakachotumika kuzipongeza shule, walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani huo.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa mkoa alisema zawadi ya gari haitatolewa kwa kuwa hakuna shule iliyoingia katika 10 bora za kitaifa.

“Kwa sasa mkoa utatoa zawadi za kawaida hadi hapo shule zitakapofanya vizuri zaidi mkoa utatoa zawadi ya gari kwa shule zitakazoingia kwenye 10 bora za kitaifa na hili linawezekana,” alisema Kanali Mtambi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu, Mwalimu Makwasa Bulenga, alisema mkoa huo ulikuwa na wanafunzi 4,708 waliofanya mtihani huo kutoka shule za sekondari 29 na wote wamepata ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu.

Matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA) Julai 7, 2025 yanaonesha kuwa shule iliyoongoza mkoani Mara kwa ufaulu ni Sekondari ya Bunda iliyopo wilayani Bunda, ambayo imeshika nafasi ya 25 kitaifa na nafasi ya saba kwa shule za serikali kitaifa, ikifuatiwa na Shule ya Sekondari Mkono ya wilayani Butiama na Shule ya Sekondari ya Tarime iliyopo wilayani Tarime.

Waliopata ufaulu wa daraja la kwanza katika shule za sekondari Bunda na Mkono ni asilimia 91 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo.

Shule za sekondari Mkono, Morembe Day iliyopo Manispaa ya Musoma, Busegwe, Chiefu Ihunyo na Kiagata za wilayani Butiama na Nyamunga iliyopo wilayani Rorya, wanafunzi wake wamepata ufaulu wa daraja la kwanza na la pili pekee.

Kwa mujibu wa Mwalimu Bulenga, asilimia 45 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo walichaguliwa kuanza kidato cha tano wakiwa na ufaulu wa daraja la tatu na wengi wao sasa wamepata daraja la kwanza na la pili.

Alisema mkoa wa Mara umepata ufaulu wa asilimia 100, huku ukiwa na wastani wa GPA 2.059 na kwamba kati ya shule 29 zilizoshiriki mtihani huo, 23 ni za serikali na za binafsi ni sita.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages