NEWS

Thursday 1 October 2020

Wanasiasa wakumbushwa kuepuka vurugu kwenye uchaguzi

Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Simiyu, Maganga Simon (aliyesimama) akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa uchaguzi mjini Bariadi, jana.

VIONGOZI wa vyama vya siasa, wagombea na wananchi kwa jumla wamekumbushwa kuendelea kufuata sheria za nchi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na kujiepusha na vitendo vya vurugu kwa kisingizio cha uchaguzi.

 Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini, Baraka Leonard, wakati akisoma hotuba ya Mwenyekiti wa Tume hiyo kwenye ufunguzi wa mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika mjini Bariadi, Simiyu jana.

 “Niwahakikishie wananchi kuwa Tume ya Uchaguzi imejipanga kusimamia uchaguzi mkuu Oktoba 28, 2020 kwa kufuata katiba, sheria na miongozo iliyopo na tuna Imani kila mdau atatimiza wajibu wake katika hili,” amesema Leonard na kuongeza:

 “Nivitake vyama vya saisa na wagombea kuzingatia maadili ya uchaguzi katika kampeni zao ikiwemo kuepuka lugha za kashfa na uchochezi, kuepuka kufanya kampeni zinazoashiria ubaguzi kwa misingi ya jinsi, ulemavu, ukabila, udini, maumbile na rangi.”

Amewatoa hofu wapigakura wote wenye mahitaji maalumu kuwa tayari maelekezo yametolewa kwa wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwa wenye ulemavu, wajawazito, wanawake wanaonyonyesha, waliokwenda na watoto vituoni, wazee na wagonjwa.

 Aidha, Leonard amewakumbusha wapigakura kujitokeza na kadi zao kupiga kura siku ya Oktoba 28, 2020 katika kituo walikojiandikisha ili kutimiza haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka kwa nafasi za urais, ubunge na udiwani.


 Kwa upande wake, Afisa Elimu ya Mpigakura kutoka NEC, Nuru Riwa, amesema Tume hiyo itaandaa hiyo jalada la nukta nundu (tactile ballot folder) kwa kila kituo cha kupigia kura kwa ajili ya wasiiona na kwamba wenye ulemavu mwingine wameandaliwa mazingira rafiki ya kupiga kura.

 Kwa mujibu wa Riwa, upigaji kura utafanyika katika vituo 80,155 vitakavyosimamiwa na kuongozwa na maofisa 320,620 walioidhinishwa na NEC.


Awali, mjumbe kutoka Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Mkoa wa Simiyu, Alex Benson ameiomba NEC kuweka mazingira rafiki kwa wasiosikia ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo ikiwa ni pamoaja na kuwawekea wataalamu wa lugha ya alama vituoni.

 Akichangia mada kwenye mkutano hao wa wadau wa uchaguzi, Semeni Kingi ambaye ni mwakilishi wa kundi la watu wenye ualbino, ameiomba NEC kuhakikisha majina ya wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani yanaandikwa kwa herufi kubwa kwenye karatasi za kupigia kura ili kuwarahisishia wenye uoni hafifu kusoma kiurahisi.

 (Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Simiyu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages