NEWS

Saturday 28 November 2020

Sh bilioni 70.5 kujaza maji Butiama, Musoma Vijijini

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) na Meneja wa Kampuni ya UNIK Construction Company Nchini Tanzania, He Yifeng, wakisaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa Sh bilioni 70.5 wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika wilaya za Musoma Vijijini na Butiama.


SERIKALI imesaini mkataba na Mkandarasi - Kampuni ya UNIK Construction Company kutoka nchini Lesotho kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika wilaya za Butiama na Musoma Vijijini - wenye thamani ya Sh bilioni 70.5.

 

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo mkoani Mara Novemba 18, 2020, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, amesema mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ambao ni Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (SFD).

 

“Mradi tuliosaini leo thamani yake ni shilingi bilioni 70.5 na ni fedha za Serikali ya Tanzania; nina kila sababu ya kumshukuru Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli kwa kutuletea fedha hizi kwa ajili ya kuhakikisha unajengwa,” amesema Mhandisi Sanga.

 

Amebainisha kwamba mradi huo utajengwa kwa miezi 24 na amemtaka Mkandarasi kuhakikisha anaukamilisha kwa wakati, hasa ikizingatiwa kuwa maandalizi muhimu yamekamilika na hakuna sababu ya kuchelewa.

 

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Maji amesema kwa kawaida huwa baada ya kusaini mkataba mkandarasi hupewa siku 30 kujipanga lakini kwa sasa utaratibu ni kwamba anapaswa kuanza kazi mara moja, hasa ikizingatiwa kuwa tayari anaelewa anachopaswa kufanya.

 

“Serikali ya Awamu ya Tano ni ya vitendo, hakuna sababu ya Mkandarasi kutumia mwezi mzima kujipanga kwani tayari hadi anasaini mkataba anaelewa kinachotakiwa kufanywa; maelekezo ya serikali ni kwamba mradi ukamilike kwa wakati,” amesisitiza.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto), akibadilishana mkataba wa ujenzi wa mradi wa kupeleka maji katika wilaya za Musoma Vijijini na Butiama na Meneja wa Mkandarasi - Kampuni ya UNIK Construction Company, He Yifeng.


 

Mhandisi Sanga amesema katika ujenzi wa miradi, serikali inazingatia vigezo vikubwa vitatu ambavyo ni ubora, gharama nafuu na muda wa utekelezwaji, yaani unapaswa ukamilike kwa wakati, hivyo amemtaka Mkandarasi kuhakikisha vigezo hivyo vinazingatiwa.

 

“Kwa vigezo hivi nilivyovitaja tayari kigezo cha gharama nafuu tumekizingatia na sasa tumebakiza hivyo viwili. Kwa hiyo ninamsisitiza Mkandarasi kuhakikisha anavizingatia na itakuwa vyema endapo atakamilisha mradi kabla ya muda huo wa miezi 24,” ameelekeza Mhandisi Sanga.

 

Amesema ujenzi wa mradi huo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa wananchi wa Butiama na Musoma Vijijini na kwamba Wizara ya Maji itahakikisha hakuna kikwazo kitakachokwamisha wala kuchelewesha utekelezwaji wake.

 

“Wananchi wanausubiri kwa hamu kubwa mradi huu kama walivyoahidiwa na viongozi wetu, sasa sisi kama Wizara ya Maji katika hili hatutokubali uzembe wa aina yoyote ile, tunachotaka ni kuona unakamilika kwa wakati na kwa ubora utakaoakisi gharama halisi ya fedha itakayotumika,” amesisitiza Mhandisi Sanga na kuwataka watendaji wa wizara yake kubaki mkoani Mara ili kuhakikisha Mkandarasi anakabidhiwa eneo la ujenzi wa mradi ndani ya saa 24 na kuanza kazi.

 

Aidha, Mhandisi Sanga amemtaka Mkandarasi kuwapa kipaumbele cha ajira wananchi wa maeneo ya mradi, hususan kwenye shughuli ambazo wanazimudu na pia ametoa wito kwa wananchi watakaopata fursa hiyo kuhakikisha wanakuwa waadilifu na wanashirikiana na mkandarasi kuulinda mradi.

 

“Ninaamini zipo shughuli nyingi ambazo wananchi wa maeneo ya mradi wanaweza kufanya, hivyo sitarajii kusikia hawapati fursa hizo na pia sitarajii kusikia wananchi wanakwamisha mradi kwa namna yoyote ile,” amesema.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi mkubwa wa maji utakaogharimu Sh bilioni 70.5 kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika wilaya za Musoma Vijijini na Butiama.


 

Aidha, Mhandisi Sanga amewakumbusha wananchi kuzingatia maelekezo ya Rais Magufuli ya kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.

 

Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya UNIK Construction Company Nchini Tanzania, He Yifeng, amemhakikishia Katibu Mkuu, Mhandisi Sanga, kwamba watatekeleza mradi huo kwa kuzingatia mkataba na maelekezo ya serikali.

 

Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji kutoka Wizara ya Maji, Mhandisi Abbas Pyarali, amesema eneo lenye mtandao wa maji safi litaongezeka kufikia asilimia 100 kwa miji ya Mugango, Kiabakari na Butiama na kwamba zaidi ya wakazi 165,000 watapata huduma ya maji kwa asilimia 100.

 

Mhandisi Pyarali alitaja maeneo yatakayonufaika kwenye awamu ya kwanza ya mradi huo kuwa ni miji ya Mugango, Kiabakari, Butiama na vijiji vya Kwibara, Nyamisisi, Kiabakari, Singu, Mwanzaburiga, Kyawazaru, Kamugegi, Kyatungwe, Ryamugabo, Bumangi, Bisarye, Tiring’ati, Butiama, Rwamkoma, Buturu, Nyang’oma, Mayani, Katalyo na Tegeruka.

 

Halfa ya utiaji saini imeshuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini, wakuu wa wilaya, Anna-rose Nyamubi (Butiama) na Dkt Vincent Naamo (Musoma Vijijini), viongozi wa kata na vijiji vitakavyonufaika na mradi huo.

 

Utiaji saini wa mradi huo mkubwa wa maji ni wa kwanza kutekelezwa tangu kuanza kwa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages