NEWS

Wednesday 25 November 2020

‘K’, Komote wang’ara uenyekiti Tarime Mjini, Vijijini

Diwani mteule wa Kata ya Nyakonga, Simon K. Samwel (kulia) akizungumza baada ya kuchaguliwa kugombea uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime leo jioni.

 

DIWANI mteule wa Kata ya Nyakonga, Simon K. Samwel, amechaguliwa kugombea uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), huku Diwani mteule wa Kata ya Nkende, Daniel Komote akichaguliwa kugombea nafasi kama hiyo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, mkoani Mara.

Diwani mteule wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye (aliyesimama) akizungumza baada ya kura zake za kugombea uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kutotosha, ambapo ameahidi kushirikiana na madiwani wote kushughulikia maendeleo ya wananchi jimboni humo.

 

Katika uchaguzi huo uliofanywa na madiwani wateule wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo jioni Novemba 25, 2020, Samwel maarufu kwa jina la ‘K’ ameibuka mshindi kwa kupata kura 21 dhidi ya Diwani mteule wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye aliyepata kura 13 na John Bosco kutoka Kata ya Regicheri ambaye hakupata kura baada ya kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho wakati wa kuomba kura ukumbini.

Diwani mteule wa Kata ya Nkende, Daniel Komote (kushoto) akizungumza baada ya kuchaguliwa kugombea uenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime leo jioni.


Kwa upande wake, Komote amevuna kura saba na kuwashinda Diwani mteule wa Kata ya Bomani, Msety Gotora aliyepata kura nne na Daudi Ngamia wa Kata ya Kitare ambaye naye hakupata kura baada ya kujiondoa kwenye mchuano huo wakati wa kuomba kura.

 

Kwa upande mwingine, madiwani wateule waliochaguliwa kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti ni Thobias Ghati (Mjini) na Victoria Mapesa (Vijijini), na waliochaguliwa kugombea nafasi ya katibu wa madiwani ni Ayub Marwa (Vijijini) na Salim Abubakar (Mjini).

Diwani mteule wa Viti Maalumu, Victoria Mapesa (kulia) akizungumza baada ya kuchaguliwa kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini leo jioni.

 

Uchaguzi huo umesimamiwa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mara, Ghati Abubakar, ambaye amewataka madiwani wote kuungana na kushirikiana na watumishi wa halmashauri zao katika kushughulikia maendeleo ya wananchi.

Mgombea uenyekiti wa Halmashauri ya Wialaya ya Tarime, Simon K. Samwel, akizungumza baada ya kuchaguliwa leo jioni.

 

Akizungumza baada ya kuchaguliwa kugombea uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ‘K’ amesema ushindi wake ni wa madiwani wote na ameahidi kusimamia miradi ya maendeleo itekelezwe kila kata bila upendeleo.

 

“Nitatanguliza maslahi ya wananchi na Chama Cha Mapinduzi ili tusije kuaibika mwaka 2025. Nitafanya ziara za kuhamnasisha maendeleo kila kata,” ameongeza diwani mteule huyo wa kata ya Nyakonga.

Madiwani wateule na wananchi wakifuatilia uchaguzi wa wagombea wa nafasi za uenyekiti, makamu mwenyekiti na katibu wa madiwani wa halmashauri za Wilaya ya Tarime na Mji wa Tarime leo jioni.

 

Naye Komote ameahidi kuimarisha umoja na ushirikiano wa madiwani kwa ajili ya kuijenga Halmashauri ya Mji wa Tarime na kuwezesha wananchi kuvuna matunda ya uongozi wao.

 

Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, amewahimiza madiwani hao kuhakikisha wanawatua wananchi mizigo ya matatizo yanayowanyima maendeleo akisema kwa kufanya hivyo watakuwa wamejinyooshea mapito ya kuchaguliwa tena mwaka 2025.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Daudi Ngicho (aliyesimama) akizungumza baada ya uchaguzi wa wagombea nafasi za uenyekiti, makamu mwenyekiti na katibu wa madiwani wa halmashauri za Wilaya ya Tarime na Mji wa Tarime leo jioni.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Daudi Ngicho, amesema yeye ametimiza jukuu lake la kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi, hivyo kazi iliyobaki ni ya madiwani na wabunge kuwaletea wananchi maendeleo waliyowaahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020.

 

“Nendeni mkawatumikie wananchi, msiwe mapilato wa kutoza wananchi ushuru, nendeni mkabuni vyanzo vya mapato na miradi ya maendeleo kwenye maeneo yenu ya uongozi,” amesisitiza Ngicho.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye maarufu kwa jina la Namba Tatu.

 

Wakati huo huo, madiwani na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wa halmashauri za wilaya, mjini na manispaa mkoani Mara, wamempongeza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye maarufu kwa jina la Namba Tatu kwa kutoingilia kwa namna yoyote chaguzi hizo.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages