NEWS

Monday 23 November 2020

VIFAFIO yataka utafiti upungufu wa samaki Ziwa Victoria

Sato ni miongoni mwa aina nyingi za samaki wanaopatikana katika Ziwa Victoria

 

SHIRIKA la Wakulima na Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria (VIFAFIO) limetoa wito kwa wadau kufanya utafiti wa kisayansi kuhusu dalili za kupungua kwa samaki katika maeneo ya ziwa hilo.

 

“Tupo ziwani [ukanda wa Ziwa Victoria] lakini hatupati samaki,” Meneja Miradi wa VIFAFIO, Majura Maingu, ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu, hivi karibuni.

Sehemu ya Ziwa Victoria jijini Mwanza


Maingu amefafanua kuwa wananchi wanaotegemea uvuvi kujipatia kipato wameanza kulalamika kuhusu kupugua kwa samaki katika ziwa hilo.

 

Amesema kupungua kwa samaki kunahusishwa na ongezeko la mimea vamizi, hususan magugumaji katika maeneo ya uvuvi.

 

“Tunahitaji utafiti wa kisayansi ufanyike ili kubaini kama kupungua kwa samaki katika Ziwa Victoria kuna uhusiano na magugumaji. Ukweli wa jambo hili lazima uthibitishwe na utafiti wa kisayansi,” amesisitiza Maingu.

 

VIFAFIO ni shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi na wakulima, wafugaji na wavuvi kwa kuwajengea uwezo ili kutumia rasilimali zinazowazunguka kuboresa maisha yao kwa uendelevu.

Wavuvi wakiwa kazini katika Ziwa Victoria

 

Uvuvi ni miongoni mwa shughuli kubwa za kiuchumi kwa maelfu ya wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria.

 

Kwa mujibu wa Maingu, VIFAFIO inashughulikia pia masuala uhifadhi na ulinzi wa vyanzo vya maji ikiwemo mto Mara na Ziwa Victoria.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages