
Mwenyekiti wa MRPC, Mugini Jacob, akifungua Mkutano Mkuu Maalum wa klabu hiyo kwenye Hoteli ya Goldland mjini Tarime, Mara jana Septemba 16, 2025.
Na Christopher Gamaina
Tarime
-----------
Wadau wa maendeleo, Soya One na Nicolaus Chichake, wameshiriki kwa hali na mali katika Mkutano Mkuu Maalum wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC) - uliofanyika kwa mafanikio makubwa mjini Tarime jana Septemba 16, 2025.
Wadau hao walitoa ufadhili uliochangia kufanikisha mkutano huo, na baadhi yao kupata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari waliohudhuria, ambapo walieleza dhamira yao ya kuunga mkono maendeleo ya sekta ya habari na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Chichake ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni za Kemanyanki Contractors Manpower and Supply Ltd na Chichake Sports Bar & Grill zenye makao makuu Nyamongo wilayani Tarime, alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kujikita katika uandishi bora na ubunifu ili kuvutia wasomaji na kujijengea heshima kwenye jamii.
Alisema angependa kuona waandishi wa habari wakikua kiuchumi kwa kutumia taaluma yao vizuri, akisema hilo linawezekana kwa kuandika habari zenye upekee na mvuto kwa wasomaji.

Chichake akizungumza kwenye mkutano huo.
“Waandishi wa habari angalieni mnatoka vipi kimaisha – msogee kiuchumi, mjipende muishi maisha ya furaha. Andaeni taarifa kwa weledi zishawishi wateja. Uandishi mzuri ni wa ku- balance stories,” Chichake alisema.
Aidha, aliwaomba wanahabari hao kuendelea kutangaza fursa za maendeleo zilizopo katika mkoa wa Mara ili kuvutia na kushawishi wawekezaji zaidi kutoka ndani na nje ya mkoa huo.
Naye Msemaji wa Soya One Limited, Mwita Meck - maarufu kwa jina la Meya, alisema kampuni hiyo ni mdau mkubwa wa waandishi wa habari, ndio maana imeona umuhimu wa kushiriki kwa hali na mali kwenye mkutano huo.
Meck ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Sabasaba mjini Tarime, aliongeza kuwa kampuni hiyo ya uchimbaji madini imekuwa ikitoa misaada ya kijamii kwa wahitaji, ikiwa ni pamoja na chakula kwa wanafunzi shuleni na wagonjwa hospitalini.

Msemaji wa Soya One, Deo Meck, akizungumza kwenye mkutano huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa MRPC, Mugini Jacob, aliwashukuru wadau hao na wengine ambao hawakufika - kwa mchango wao muhimu, akiwataja kama “wadau wa kweli wa maendeleo ya tasnia ya habari mkoani Mara.”
Mugini alisisitiza kuwa MRPC inathamini ushirikiano inaopata kutoka kwa wadau hao, na akatumia nafasi hiyo pia kuwaomba waandishi wa habari mkoani Mara kuwapa ushirikiano kila unapohitajika.
Alisema wadau hao - Soya One na Chichake, wameonesha mfano wa kuigwa katika kushirikiana na waandishi wa habari kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi mkoani Mara.

Mwenyekiti wa MRPC, Mugini Jacob, akizungumza katika mkutano huo.
Mikutano ya MRPC imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kujadili maendeleo ya waandishi wa habari, changamoto zao na namna ya kuboresha tasnia hiyo ili iendane na matakwa ya dunia ya sasa ya kidigitali na ushindani wa habari.
No comments:
Post a Comment