Mkulima na mkazi wa kijiji cha Mara-Sibora, Akuti Atieno akionesha sehemu ya shamba aliloanza kuandaa jirani na Mto Mara |
MAFURIKO yaliyotokea Aprili na Mei mwaka huu, yalisababisha madhara makubwa kwa wakulima, wafugaji na wachimbaji madini kandokando ya Mto Mara nchini Tanzania.
Uchunguzi uliofanywa na Mara Oline News katika maeneo hayo hivi karibuni, umebaini kuwa mafuriko hayo yalisomba mazao mbalimbali ya chakula na biashara na kuwaacha wakulima bila mavuno.
Baadhi ya mazao yaliyosombwa na mafuriko hayo katika maeneo oevu ya Mto Mara ni pamoja na mahindi, mhogo, mtama na mbogamboga.
Wakulima walioathiriwa na mafuriko hayo hivi sasa wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kwani hawakuwa na akiba ya chakula baada ya mazao waliyotegemea kuvuna kusombwa mashambani.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa jumuia ya watumia maji ukanda wa Mara Kaskazini, Siproza Charles, mafuriko hayo yalisomba mazao mbalimbali katika mashamba yanayokadiriwa kuwa na ukubwa wa ekari 400 katika eneo oevu la mto Mara katika Kijiji cha Mara-Sibora.
Mkulima na mkazi mwingine wa kijiji cha Mara-Sibora, Siproza Charles akielezea madhara waliyopata kutokana na mafuriko kijijini hapo.
Katika baadhi ya maeneo mifugo kadhaa wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo iliripotiwa kusombwa na mafuriko yaliyojaa ghafla kwenye mazizi.
Mafuriko hayo yalikwaza pia shughuli za uchimbaji madini zinazoendeshwa jirani na Mto Mara kutokana na maji kujaa kwenye mashimo husika.
Vijiji vilivyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo ni Mara-Sibora, Matongo, Kerende, Nyabichune, Bisarwi, Wegita, Buswahili na Wegero vilivyopo katika wilaya za Tarime, Butiama na Musoma mkoani Mara.
Mafuriko hayo yalitokea kipindi ambacho mlipuko wa janga la virusi vya Corona ulikuwa umeripotiwa katika baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.
Hata hivyo, ugonjwa huo wa Corona haukuwafikia wananchi hao wanaoishi na kuendesha shughuli za kilimo, ufugaji na uchimbaji madini kandokando ya Mto Mara.
Mojawapo
ya mashamba yaliyoandaliwa kwa ajili ya kupandwa mazao jirani na mto Mara
katika kijiji cha Mara-Sibora.
Licha ya kuhofia mafuriko mengine, baadhi ya wananchi hivi sasa wameanza kulima mashamba na kupanda tena mazao ya chakula katika maeneo oevu ya Mto Mara, kwa kuwa hawana namna nyingine wanayotegemea kuendesha maisha yao zaidi ya kilimo.
Kwa mujibu wa wataalamu kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), mafuriko ya Aprili na Mei mwaka huu yalisababishwa na mvua nyingi zilizonyesha kwa miezi kadhaa mfululizo na kujaza maji ndani na nje ya Mto Mara.
“Mvua zilikuwa nyingi, na sio Mto Mara pekee uliojaa maji, bali hata Ziwa Victoria mafuriko yalivunja rekodi,” Mhaidrojia wa LVBWB, Wiston Agwaro ameiambia Mara Online News.
Kimsingi, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini pia kwamba wananchi wanaoishi na kulima jirani na Mto Mara hawana uelewa wa kutosha juu ya athari za mafuriko na hata suala zima la kuchukua tahadhari ya janga hilo la asili.
Shemu
ya eneo oevu la Mto Mara katika wilaya ya Butiama mkoani Mara linalotumika kwa
shuguli za kilimo na malisho ya mifugo.
Wananchi hao wanasema wamekuwa wakiendesha shughuli za kilimo katika maeneo hayo miaka mingi na hawakuwahi kuelezwa madhara yake wala kuzuiwa na mtu yeyote yule.
Kwa mantiki hiyo, kuna haja ya wataalamu wa masuala ya mafuriko kuelekeza elimu juu ya madhara na tahadhari ya janga hilo kwa wakulima na wakazi wa kandokando ya mto Mara iwasaidie kuepuka madhara ya aina hiyo siku za mbeleni.
Ni vizuri wataalamu hao washirikishe viongozi wa serikali ambao wana jukumu la kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya kitaalamu na kisheria ikiwemo kuhakikisha wananchi hawalimi na kuishi katika maeneo oevu ya Mto Mara.
Ni wazi kwamba wananchi hao wakielimishwa kuhusu madhara ya kulima na kuishi jirani na mto huo watachukua hatua za tahadhari kwa kuwa hakuna aliye tayari kuathiriwa kwa namna yoyote ile na mafuriko.
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment