NEWS

Wednesday 23 December 2020

Grumeti Fund yawapa wanavijiji suluhisho la wanyamapori waharibifu

Meneja Uhusiano wa Grumeti Fund, David Mwakipesile akiwasilisha mada wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanavikundi vya kudhibiti wanyamapori waharibifu katani Mugeta.
 

KAMPUNI ya Grumeti Fund imeandaa na kuwezesha mafunzo ya kuvijengea uwezo vikundi vya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wa mazao ya chakula na biashara katika vijiji vinne vinavyounda kata ya Mugeta wilayani Bunda, Mara.

 

Mafunzo hayo yamewakusanya pamoja wanavikundi 54 kutoka vikundi vinne vya kudhibiti wanyama hao katani humo, leo Desemba 23, 2020.

 

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Serengeti, Lawrent Katakweba, amesema dhumuni kuu ni kuwafundisha mbinu za kusaidia wananchi kufukuza wanyamapori waharibifu kabla hawajasababisha madhara vijijini.

Mkuu wa Kikosi cha Kudhibiti Ujangili Kanda ya Serengeti, Lawrent Katakweba akifungua mafunzo ya kuvijengea uwezo vikundi vya kudhibiti wanyamapori waharibifu katani Mugeta.

Katakweba amefafanua kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa kushirikisha wadau wa uhifadhi na wananchi katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wa mazao katika vijiji vinavyopakana na maeneo ya uhifadhi.

Baadhi ya wanavikundi wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kudhibiti wanyamapori waharibifu katani Mugeta.
 

“Serikali yetu inajali sana wananchi kuliko wanyamapori, lakini inabidi (wanyamapori) waendelee kuwepo kwani wana umuhimu katika ikolojia na wanachangia pato la Taifa kutokana na utalii.

 

“Ifahamike pia kwamba wanyamapori wakali na waharibifu kama vile tembo, viboko, mamba na simba ndio wanapendwa sana kutazamwa na watalii wengi.

 

“Kwa hiyo, mpango huu wa serikali ni kuhakikisha wanyama hawa wanakuwepo na maisha ya binadamu yanaendelea,” amesisitiza Katakweba.


Meneja Uhusiano wa Grumeti Fund, David Mwakipesile amesema kata ya Mugeta imestahili kupewa mafunzo hayo kwa kuwa ni ya pili kwa kuathiriwa zaidi na wanyamapori waharibifu ikitanguliwa na kata ya Hunyari wilayani Bunda.

Meneja Uhusiano wa Grumeti Fund, David Mwakipesile akiendelea kutoa mafunzo ya kuvijengea uwezo vikundi vya kudhibiti wanyamapori waharibifu katani Mugeta.

Wanyamapori waharibifu wanaovamia vijiji na kuharibu mazao mbalimbali mashambani wamekuwa wakitoka katika mapori ya akiba ya Ikorongo, Grumeti na Ikona WMA lililotengwa na wananchi kwa ajili ya kutunza wanyamapori ili kuwaingizia kipato cha fedha.

Sehemu nyingine ya washiriki hao wa mafunzo ya kujengewa uwezo wa kudhibiti wanyamapori waharibifu katani Mugeta.
 

Mwakipesile amesema tatizo hilo limetokana na ongezeko la idadi ya watu na baadhi yao kusogelea maeneo ya uhifadhi kwa kuishi na kulima kwenye mapito ya wanyamapori.

 

Amesema Grumeti Fund inashirikiana na serikali katika uhifadhi wa wanyamapori na maendeleo ya wakazi wa vijiji vinavyopakana na maeneo ya uhifadhi.


Naye Mhifadhi Wanyamapori kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Herry Christopher amesema kata ya Hunyari inayoongoza kwa kuathiriwa zaidi na wanyamapori waharibifu ina vikundi 21 vya kudhibiti wanyama hao ikifuatiwa na kata ya Mugeta yenye vikundi vinne.

Mhifadhi Wanyamapori kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Herry Christopher akieleza majukumu ya vikundi vya kudhibiti wanyamapori waharibifu katani Mugeta.

“Wajibu mkubwa wa vikundi hivi ni pamoja na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka za uhifadhi kabla wanyamapori waharibifu hawajasababisha madhara vijijini,” amesema Christopher.

Wawezeshaji wa mafunzo ya kudhibiti wanyamapori waharibifu (waliokaa) katika picha ya pamoja na wanavikundi waliopewa mafunzo hayo katika kata ya Mugeta wilayani Bunda.


(Habari na picha zote na Mara Online News)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages