NEWS

Tuesday 29 December 2020

Hifadhi ya Serengeti ilivyowezesha miradi ya kijamii na kiuchumi katika wilaya za Ngorongoro na Serengeti

Mhifadhi Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hobokela Richard (kushoto), akifafanua jambo kwa viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Park Nyigoti wilayani Serengeti - akiwemo Mwenyekiti, Mtiro Kitigani (kulia), walipokwenda kukagua mradi wa lambo la maji ya mifugo kijijini hapo, hivi karibuni. Lambo hilo lililochimbwa kwa kutumia mtambo uliotolewa na Hifadhi hiyo.
 

MATUNDA ya uhifadhi yamedhihirika katika wilaya za Serengeti na Ngorongoro baada ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuwezesha uanzishaji miradi ya ufugaji nyuki, ujenzi wa zahanati na lambo la maji ya mifugo.

 

Katika wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Mwenyekiti wa vikundi vya ufugaji nyuki, Isaya Ole Seki, anasema Hifadhi hiyo kupitia idara yake ya ujirani mwema, imewezesha uanzishaji wa miradi minne ya ufugaji huo katika eneo la Loliondo.

 

“Vikundi vyote vilianza mwaka 2018 baada ya Hifadhi kuwezesha wanavikundi mafunzo ya ujasiriamali, misaada wa mizinga 30 kwa kila kikundi na vifaa kazi vikiwemo vya kurinia asali,” anasema Ole Seki katika mahojiano na Mara Online News wilayani humo, hivi karibuni.

Mwanachama wa kikundi cha wafugaji nyuki katika eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro akieleza watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (hawapo pichani) jinsi walivyojipanga kuendeleza ufugaji huo kwa tija.

Ole Seki anasema miradi hiyo itakuwa endelevu - ikilenga kuwapatia wanavikundi kipato cha fedha kwa ajili ya kukabili mahitaji mbalimbali katika familia zao.

 

“Soko la asali lipo, uhusiano na Hifadhi ni mzuri na sisi wananchi tunaona faida ya uhifadhi,” anasema Mwenyekiti huyo.

Mhifadhi Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hobokela Richard (wa pili kushoto), akifafanua jambo kwa baadhi ya wanachama wa vikundi vya ufugaji nyuki - Loliondo wilayani Ngorongoro, hivi karibuni.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikundi cha ufugaji nyuki cha Naisho, Moses Kitupei, anasema wameanza kurina asali na kuuza, japokuwa wanakabiliwa na uchakavu wa vifaa kazi.

 

Mwanachama wa kikundi cha Uhifadhi na Maendeleo, Naiyolo-gug Kursas, anaishukuru Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kuwawezesha kuanzisha ufugaji huo akisema utawaongezea kipato kitakachowasaidia kumudu gharama za mahitaji ya shule ya watoto wao.

Wanachama wa kikundi cha ufugaji nyuki cha Uhifadhi na Maendeleo akiwemo Naiyolo-gug Kursas (kulia), wakionesha mzinga kati ya 30 waliyowezeshwa na Haifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Naye Joseph Killel kutoka kikundi cha Ardhi ni Mali, anasema ufugaji huo wa nyuki unasaidia pia kuhifadhi misitu na mazingira kwa ujumla katika maeneo yanayopakana na Hifadhi.

 

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Lorien/ Magaiduru, Agnes Thamas, anasema elimu zaidi ya uhifadhi inahitajika kwa wakazi wa vijiji jirani kwa ajili ya uhifadhi endelevu wa wanyamapori na mazingira.

Simba akiwa amejipumzisha ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Kwa upande mwingine, Hifadhi ya Serengeti imewezesha ujenzi wa zahanati na nyumba ya waganga wawili katika kijiji cha Losoito wilayani Ngorongoro, ambayo inasubiri vifaa tiba kwa ajili ya kuanza huduma kwa wananchi.

Jengo la zahanati ya kijiji cha Losoito wilayani Ngorongoro lililojengwa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa ushirikiano na wakazi wa kijiji hicho.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pia imeshirikiana na wananchi kujenga nyumba ya kuishi itakayotumiwa na waganga wawili wa zahanati ya kijiji cha Losoito wilayani Ngorongoro, Arusha.

Kiongozi wa Kimila wa kabila la Wamasai, Lakakui Kantoli, anayejulikana zaidi kama Laigwanan, anasema zahanati hiyo itawaondolea wakazi wa kijiji hicho adha ya kusafiri umbali wa kilomita 30 kwenda kijiji jirani kutafuta huduma za matibabu.

 

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Losoito, Michael Peliay, anasema baadhi ya wajawazito wamekuwa wakipoteza maisha wakiwa njiani kupelekwa kutafuta huduma katika eneo la Loliondo.

Mwandishi wa Mara Online News, Christopher Gamaina (katikati), akifanya mahojiano na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Losoito wilayani Ngorongoro, Arusha kuhusu mradi wa zahanati ya kijiji hicho uliotekelezwa kwa ushirikiano na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
 

Naye mkazi wa kijiji hicho, Tenanai Koreta, anasema wanakijiji waliibua mradi wa zahanati hiyo mwaka 2017 na kuchangia nguvu kazi iliyohusisha kusomba mawe, mchanga, matofali, kokoto na maji.

 

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Taka, anaishukuru Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kushirikiana na wananchi katika kutekeleza miradi ya kijamii na kiuchumi, huku akiiomba kupanua wigo wa kuwawezesha kunufaika zaidi na ‘keki’ ya uhifadhi.

 

Katika wilaya ya Serengeti, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kupitia idara yake ya ujirani mwema imewezesha utekelezaji wa mradi wa lambo la maji ya mifugo katika kijiji cha Park Nyigoti. Mtambo wa kulichimba ulitolewa na Hifadhi hiyo.

Lambo la maji ya mifugo katika kijiji cha Park Nyigoti lililochimbwa kwa kutumia mtambo uliotolewa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Mtiro Kitigani, anasema “Pamoja na changamoto zilizopo, tumenufaika na uhifadhi ikiwa ni pamoja na kusaidiwa katika ujenzi wa shule na zahanati ya kijiji na wanafunzi wanasomeshwa hadi vyuoni.”

 

Viongozi na wakazi wa kijiji hicho wanaishukuru Hifadhi hiyo kwa msaada huo na kuomba iendelee kuwakumbuka katika miradi mingine ya kijamii na kiuchumi, huku wakiahidi kushirikiana nayo katika kudhibitoi vitendo vya ujangili hifadhini.

 

Mhifadhi Ujirani Mwema wa Hifadhi hiyo, Hobokela Richard, anasema wanaendelea na juhudi za kupanua wigo wa kuwezesha wakazi wa vijiji vilivyo jirani kunufaika zaidi na fursa za uhifadhi na utalii.

 

(Imeandikwa na Christopher Gamaina)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages