Sehemu ya kingo za Mto Mara zinavyoonekana baada ya ukataji miti. |
MTO Mara ni muhimu kwa shughuli mbalimbali za binadamu zikiwemo za kilimo cha umwagiliaji, maji kwa ajili matumizi ya nyumbani, mifugo na uvuvi, hususan kwa wakazi wa vijiji jirani na bonde la mto huo.
Licha yam to huo kuwa muhimu kwa maisha ya binadamu, bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazosababisha bonde lake kupoteza asili yake.
Wiki iliyopita, Mara Online News ilizungumza na wakazi wa kijiji cha Matongo kilicho jirani na Bonde la Mto Mara wilayani Tarime, Tanzania.
Mara Online News ilitaka kujua kwanini miti inazidi kupotea, huku shughuli za Kilimo, matumizi ya mkaa, kuni na ujenzi vikichangia uharibifu wa mazingira katika Bondee hilo.
Magogo ya miti iliyokatwa kandokando ya Mto Mara wilayani Tarime.
Mkazi wa kitongoji cha Kegonga B kijijini Matongo, Mwita Matiko ni miongoni mwa wachomaji mkaa kwa zaidi ya mika 30 sasa, anakiri kuwa Bonde la Mto Mara linazidi kupoteza uasili wake, hasa kupungukiwa miti.
Anasema kadri miaka inavyokwenda miti kwenye Bonde hilo inazidi kupotea kutokana na ongezeko la watu linalosababisha mahitaji ya miti mingi na uharibifu wa mazingira.
“Wakati sisi tunakua watu walikuwa wachache… kufika kwa jirani yako ulitumia dakika 20 hadi 30, kulikuwa na miti mingi katika maeneo tunayoishi, haikumlazimu mtu kwenda kukata miti iliyo karibu na mto.
“Kulikuwa na vichaka vingi kwa sababu ya misitu, lakini kadri watu walivyoongezeka mahitaji nayo yakaongezeka, wengine wanakata miti ili kujenga na kupaua nyumba zao, kwa ajili ya kuni na kujenga mazizi ya ng’ombe,” anasema Matiko.
Anaongeza “Kwa wakati huo matumizi ya mkaa yalikuwa kidogo, wachache ndio walikuwa wanafanya biashara ya mkaa, wengi ilikuwa ni biashara ya kuni maana wengi walitumia kuni, hivyo miti ikapungua na kusababisha watu kwenda kuitafuta bondeni.”
Waziri wengi wa vijiji vilivyo ndani ya Bonde la Mto Mara wanatumia kuni kupika vyakula.
Mwanbakijiji mwingine, Wambura Chacha anasema ukataji miti unatokana na ugumu wa maisha na kwamba mkaa ni sehemu ya kujipatia kipato ikizingatiwa wakazi wa kijiji hicho wengi ni wakulima na wafugaji, hawana biashara nyingine.
"Mazingira tunayoishi sisi ni wakulima na wafugaji, unapolima unategemea utavuna mazao mengi lakini mvua ikinyesha kubwa vyakula vinaharibika na familia uliyonayo ni kubwa, kwa hiyo unatafuta njia mbadala ya kuishi - unakata miti anauza kwa wafanyabiashara wa mkaa ili apate fedha," anasema na kuongeza:
“Wengine hawalimi wala kufuga, uzoefu wake ni kukata miti, kuichoma na kuuza mkaa ndio maisha yake, sasa ukimzuia kukata miti bila kumpa mbadala atakushangaa na kukupuuza.”
Naye Ghati Marwa anasema “Mfanyabiashara wa mkaa hukata miti mingi kulingana na mahitaji yake ili apate fedha nyingi.”
Marwa anaongeza “Sio wote wanapenda kufanya biashara hii ya kuchoma mkaa, ni ngumu na ni gharama inahitajika, kama hauna miti inabidi uinunue na lazima utafute nyasi, udongo, utengeneze vichanja vya kuweka chini ili magogo yasiharibiwe na moto.”
Mkazi wa kijiji cha Kisaka akiangalia mazingira ya Mto Mara wilayani Tarime.
Nyabase Samson ni mzaliwa wa kijiji cha Kisaka wilayani Serengeti amabye aliolewa katika kitongoji cha Kegonga. Ni mchomaji na mfanyabiashara wa mkaa. Anasema shughuli za kilimo nazo zinachangia ukataji miti.
"Hii miti ni yetu, iko kwenye mashamba yetu, sio maeneo ya Serikali, ni miti ya asili, ukihitaji eneo la kulima inabidi ukate miti ulime. Mimi nimchomaji mkaa kwa zaidi ya miaka kumi, nina watoto sita, mkaa ndio biashara yangu, kwa siku tunachoma tanuru tatu sawa na magunia sita - gunia moja ni sawa na debe tano, gunia moja tunauza kati ya shilingi 25,000 hadi 30,000 na debe moja kati ya shilingi 4,000 hadi 5,000,” anasema Samson.
Anasema uchomaji mkaa hauna gharama bali ni nguvu za mkata miti, kuchoma na kusafirisha, “Kuna wanaochoma mkaa kule Gwikoma-Ngurimi ng’ambo ya mto na kuivusha huku kwetu, kuna wanaochoma eneo la Remorogho, Retoka, Reghati, wengine wana miti yao, wengine wananunua, wengine wanaiba kwenye mashamba ya watu, ni nguvu zako tu.
“Katika uchomaji mkaa kuna aina za miti inayofaa kwa mkaa, si kila miti inachoma mkaa kama huku kwetu tunatumia miti ambayo tunaitambua kwa kabila letu la Kikurya ambayo ni mihangate, imika, vilela, imerogho, mikuyu hatuitumii kwa sababu mikaa yake ni mibaya haiuziki na ina utomvu mwingi - ni hatari kwa mchomaji na misaghare yenyewe ina harufu kali sana japo nayo wameanza kuichoma wanaikausha juani kwanza,” anasema.
Nini kifanyike miti isikatwe?
Wanakijiji wameeleza mbinu zinazoweza kusaidia kupunguza ukataji miti ndani ya Bonde la Mto Mara kuwa ni pamoja na Serikali kupeleka umeme na elimu ya matumizi ya nishati mbadala kama gesi kwenye vijiji vilivyo jirani na bonde hilo.
‘’Sisi tuko vijijini, huwa tunasikia kwenye redio kuwa watu wamekufa kwa majiko ya gesi, hii imefanya watu kuogopa kuyatumia, watu wapewe elimu ya matumizi bora ya gesi na tuletewe umeme - itapunguza lakini sio kumaliza maana watu wana familia kubwa hawezi kupika ugali mkubwa kwenye gesi,” anasema.
Machugu anasema licha ya kuwepo Mto Mara, wananchi wanaopakana nao si wavuvi, hivyo ni vyema Serikali ikaja na mbinu ya kuwashawishi kuwa wavuvi wa dagaa, itasaidia kupunguza uchomaji mkaa.
Maji ya Mto Mara pia ni tegemeo muhimu kwa ajili ya mifugo.
Mkazi wa kijiji cha Kegonga A, Bhoke Wambura anasema “Tuletewe pembejeo za kilimo zitakazostahimili misimu yoye ya mvua na jua ili mkulima anapolima apate mazao mengi ambayo haitamlazimu kwenda kuchoma mkaa kwa kuwa atakuwa na chakula cha kutosha na kuuza kwa ajili ya familia na wawatembelee watu wanaochoma mkaa kuwapa elimu. Tunasikia Serikali inatoa mikopo lakini watu hawajui wataipata kwa njia zipi, mkaa ni matumizi ya familia nyingi haihitaji nguvu kubwa kuzuia bali ni kukaa pamoja na kutafuta njia mbadala ili kunusuru Mto Mara.”
Matitimbe Lazack anasema Serikali ikidhibiti wanaochoma mkaa kwa kuwapa elimu ya njia mbadala za kuishi itasaidia maana hakutakuwepo na wachomaji mkaa, hivyo watu watabuni njia nyingine za nishati badala ya mkaa na kuni.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kegonga B, Gachori Gachori anasema ukataji miti umeathiri Mto Mara na kuusababisha kuacha mkondo wake na kumwaga maji kwenye mashamba, kuharibu mazao na kusababisha uhaba wa chakula.
"Zamani bonde lote lilikuwa limejaa miti mbalimbali, kuna miti kwa kabila letu la Wakurya tunaiita Macheno ina mizizi mikubwa, inaota kandokando mwa mto inasaidia sana kudhibiti mmomoyoko wa udongo, ilisaidia mto kutoacha njia kwa kuwa miti ilikuwa mingi, sasa hivi hakuna miti - matokeo yaka mto ukijaa unaacha mkondo wake na kwenda kwenye mashamba nakufanya vijito vijito tunavyoviita amatura yanajaa utadhani bwawa, mazao yanapelekwa na maji,” anasema Gachori.
Anaongeza “Baadhi ya maeneo yaliyokuwa yanalimwa sasa hivi hayalimwi yameshakuwa mabwawa kwa sababu ya miti kukatwa, kwenye kitongoji changu hakuna elimu iliyotolewa kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa Bonde la Mto Mara.”
Mbali ya ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa, wanavijiji pia wamekuwa wakilima mazao ya chakula jirani na Mto Mara.
Kibwabwa Mwita ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kegonga A, anasema hawajawahi kupewa elimu na kwamba ni vyema viongozi na wananchi wakajengewa uwezo wa mbinu mbalimbali kuhakikisha biashara ya mkaa inakwisha na watu wahamasishwe kupanda miti pindi anapokata mti.
Afisa Maliasili Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Njonga Budeba anasema elimu imekuwa ikitolewa kupitia vikundi mbalimbali vya wananchi na kwambia inakuwa vigumu kumdhibiti kila mtu kutokana na miti kumilikiwa na wananchi.
"Si wengi wanaotumia mkaa kwenye hivyo vijiji, miti iko kwenye mashamba yao, wengine wanaikata kwa ajili ya mbao na kuni,I nakuwa vigumu kutumia nguvu kuwazuia kwa kuwa wao ndio wamiliki wa miti hiyo.
Anawataka wananchi kubadilika na kutumia njia nyingine za nishati kwani elimu imekuwa ikitolewa lakini baadhi yao hupuunza kwa kuwa miti ni yao. Anakiri kuwa uwepo wa miti kwenye Bonde la Mto Mara ni muhimu kwa maisha ya binadamu.
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment