NEWS

Sunday 20 December 2020

Naibu Waziri Waitara atoa maelekezo ya usalama mgodi wa Buhemba

Naibu Waziri wa Nchi, Ofsi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mwita Waitara (wa tatu kulia) akikagua shughuli za wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Mgodi wa Buhemba wilayani Butiama, Mara.


 

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mwita Waitara amewaagiza wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Mgodi wa Buhemba wilayani Butiama, Mara kuhakikisha wanavaa vifaa vya usalama muda wote wanapokuwa kazini ili kuepuka athari, au ajali zinazoweza kuwapata kutokana na kutovaa vifaaa hivyo.

 

Waitara ametoa agizo hilo alipofanya ziara mgodini hapo Desemba 19, 2020 kukagua mazingira, ambapo alikuta wachimbaji hao wakitekeleza shughuli zao bila kuwa na vifaa hivyo, yaani protective Gears.

 

Pia amewataka wachimbaji hao kuzingatia utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji miti katika maeneo hayo yasigeuke jangwa ili mgodi huo uwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

 

Katika Hilo, ameuagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kuelekeza elimu na ushauri kwa wachimbaji hao ili kuhakikisha miti wanaoyoipanda katika eneo hilo haikauki.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) akiendelea kukagua shughuli za wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Mgodi wa Buhemba.

 

“Niwaombe sana wachimbaji wa mgodi huu hakikisheni kila mtu anakuwa na vifaa vya kujikinga kwa ajili ya afya kutokana na kazi mnazozifanya, nawaagiza lazima kila mtu awe na kifaa cha kumlinda, hii ni kwa ajili ya maisha yenu,” amesisitiza Naibu Waziri huyo.

 

Mmoja wa wachimbaji hao, Hassan Rashid amekiri kuwepo kwa baadhi ya wachimbaji wadogo wasiovaa vifaa hivyo na kuahidi kushirikiana na wenzake kutekeleza agizo hilo na lile la kupanda miti na kuweka mkakati wa kukabiliana na mifugo ambayo imekuwa ikirudisha nyuma jitihada hizo.

 

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mwalimu Anna-rose Nyamubi amesema kumekuwepo na ukataji miti ovyo unaofanywa na baadhi ya wachimbaji wagodo wa madini.

 

Hata hivyo, Nyamubi amesema wanaendelea kuelimisha wachimbaji hao umuhimu wa kupanda miti na kutunza mazingira.

 

(Imeandikwa na Mussa John, Butiama)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages