NEWS

Wednesday 6 January 2021

Aweso ashusha rungu kwa kigogo RUWASA Rorya

Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso akizungumza na wakazi wa Shirati wilayani Rorya, ambapo ametangaza kumvua madaraka Meneja wa RUWASA wa wilaya hiyo, Mhandisi Evaristo Mgaya, leo Januari 6, 2021.

WAZIRI wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso, leo Januari 6, 2021 amemvua madaraka Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Rorya, Mhandisi Evaristo Mgaya, kutokana na kushindwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji wananchi wapate huduma.

 

Waziri Aweso ameshusha ‘rungu’ hilo kwa Mhandisi Mgaya ikiwa ni siku moja imepita baada ya ‘kuwatumbua’ Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mara, Mhandisi Sadick Chakka na mwenzake wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Marwa Murasa, kutokana na uzembe wa aina hiyo kwenye maeneo yao ya uongozi.

 

Kilichompoza zaidi Mhandisi Mgaya ni miradi ya maji Kirogo na Shirati ambayo utekelezaji wake umekwama na kusababisha wananchi wa maeneo hayo kuendelea kukosa huduma ya maji licha ya serikali kupeleka Sh bilioni 1.3 kwa ajili ya kugharimia ukarabati, lakini pia mamilioni kadhaa ya fedha kwa ajili ya usimamizi.

 

Imeelezwa kwamba mkandarasi wa mradi maji wa Kirogo ameshalipwa Sh bilioni moja kwa ajili ya ukarabati, lakini hadi sasa mradi huo hauoneshi dalili za kuwa msaada kwa wananchi.

 

Kwa upande wa mradi wa Shirati, imeelezwa ulisimama kufanya kazi mwaka 2016 baada ya pampu kuharibika, ambapo serikali imetoa fedha za kuuhuisha lakini bado hakuna dalili za kuanza kusambaza huduma ya maji kwa wananchi.

 

Kabla ya ‘kumtumbua Meneja huyo wa RUWASA Rorya, Waziri Aweso amempigia simu ya kiganjani Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), CPA Joyce Msiru na kumuuliza gharama anazoweza kulipwa kwa ajili ya kuhuisha mradi wa maji Shirati, ambapo amemweleza Waziri kuwa kazi hiyo inahitaji Sh milioni 247.

 

Katika mawasiliano hayo, Waziri huyo ameahidi kuipatia MUWASA kiasi hicho cha fedha na kuitaka kuanza kazi hiyo kesho Januari 7, 2021 na kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuanza kusambaza maji kwa wananchi ndani ya kipindi cha siku 30 kama ambavyo Mkurugenzi Mtendaji, CPA Msiru ameahidi.

Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso (wa pili kulia) akitoa maelekezo ya utekelezaji wa miradi ya maji wilayani Rorya, leo Januari 6, 2021. Wa tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga.

Akitoa tamko la kumng’oa madarakani Meneja huyo wa RUWASA Wilaya ya Rorya, Waziri Aweso amesema “Tumeona kuna usimamizi hafifu wa miradi ya maji licha ya serikali kuleta fedha za usimamizi, tunataka mtu anayekwenda na kasi ya Rais John Pombe Magufuli - wananchi wapate maji.”

 

“DM [akimaanisha Meneja wa RUWASA Wilaya] hapa Rorya hautufai, tafuta kazi nyingine, tutaleta mtu mwingine watu wapate maji, na wote waliochezea miradi ya maji watafikishwa polisi, wakandarasi wote waliokula fedha za maji wajiandae kuzitapika,” amesema Waziri Aweso na kuongeza:

 

“Serikali imeleta fedha nyingi za maji Rorya lakini miradi mingi imechezewa, watu wamepewa tenda kishemejishemeji, tutawashughulikia majambazi wa fedha za maji. Ninataka watu wapate maji, hiyo ndiyo faraja yangu na ya Rais John Pombe Magufuli."

Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso (katikati) akiwasili kukagua mradi wa maji Shirati wilayani Rorya, leo Januari 6, 2021. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa kwa Waziri huyo, RUWASA Wilaya ya Rorya imepokea kutoka serikalini Sh bilioni 1.3 kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya maji ili wananchi wapate huduma hiyo, lakini wameendelea kukosa huduma hiyo kutokana na usimamizi mbovu.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages