NEWS

Monday 25 January 2021

Maboresho ya kishindo yaja BRELA

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa BRELA, Godfrey Simango Nyaisa

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) iko katika hatua za mwisho za majaribio ya kubadilisha na kuboresha mfumo wake wa huduma kwa wateja kwa kuzingatia changamoto zilizopo katika mfumo unaotumika kwa sasa.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha habari na mawasiliano kwa vyombo vya habari cha BRELA leo Januari 25, 2021, mabadiliko na maboresho hayo yalianza Mei 2020 kwa kushirikiana na wataalamu wa mifumo kutoka taasisi mbalimbali za serikali.

 

BRELA imetoa ufafanuzi huo kufuatia taarifa iliyosambaa katika mitandao ya kijamii kwamba imekuwa ikikimbiza wawekezaji kutokana na changamoto za Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS).

 

Imesema mfumo mpya utakapokamilishwa utakabidhiwa kwa ajili ya kuanza kutumika rasmi huku ukisimamiwa na wataalamu wazawa tofauti na mfumo wa sasa unaosimamiwa na mzabuni kutoka nje ya nchi.

 

“Wakala inatambua dhamana iliyopewa na serikali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha shughuli za uwekezaji zinaongezeka nchini, hivyo inaendelea kufanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikionekana kuwa ni kikwazo katika urasimishaji wa biashara kupitia mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao,” imeeleza taarifa hiyo na kuendelea:

 

“Kukamilika kwa mfumo huo kutaweza kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na maombi kupokewa na kufanyiwa kazi na ofisa mmoja, kufanyiwa kazi kwa kuzingatia ombi lililofika awali, kuendelea kuunganisha mfumo wa BRELA na mifumo ya taasisi nyingine kama Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Benki, Uhamiaji na mamlaka za utoaji leseni katika halmashauri.”

 

BRELA imesema lengo kuu ni kutengeneza mazingira rafiki na wezeshi sio tu kwa wawekezaji bali wafanyabiashara wote.

 

Aidha, katika kuhakikisha kwamba kipindi hiki wadau wa BRELA wanapata huduma nzuri, Wakala hiyo imeanzisha kituo cha miito na huduma kwa wateja.

 

“Kituo hiki kazi yake kuu ni kutoa usaidizi wa haraka kwa wateja wetu wanapokwama wakati wa urasimishaji wa biashara zao.

 

“Ni vyema umma ufahamu kwamba muda wa usajili wa jina la biashara ni siku moja na si zaidi ya siku tatu za kazi na usajili wa kampuni ni siku tatu na si zaidi ya siku tano za kazi.

 

“Usajili wa alama za biashara na huduma ni kipindi cha siku 90 (kutokana na takwa la kisheria), maombi ya kupata hataza ni siku 120, kupata leseni ya kiwanda au biashara kundi A ni siku moja na si zaidi ya siku tatu za kazi.

 

“Baada ya kipindi hicho kupita kama usajili haujakamilika mteja awasiliane na kituo cha huduma kwa wateja kupitia namba: +255 (0) 222 212 800 au kwa barua pepe: maoni@brela.go.tz kwa ajili ya usaidizi wa haraka.

 

“Hivyo basi, Wakala inawataka wadau wake kufuata taratibu za usajili ikiwa ni pamoja na ujazaji wa taarifa kwa makini na uwekaji wa viambatanisho sahihi ili kuepusha kuchelewa kwa kukamilika kwa usajili.

 

“BRELA wakati wote tunapokea maoni ya wadau kwa lengo la kuboresha sio tu mifumo bali pia uendeshaji wa Taasisi yetu,” imesema taarifa hiyo na kuhitimisha kwa kaulimbiu ya BRELA: “Tunaipa utu wa kisheria biashara yako.”

 

#MaraOnlineNews - Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages