NEWS

Sunday 24 January 2021

Zahanati ya Nyagisya yanukia, DC, wanakijiji wazungumza

Mkuu wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon (kulia), akizungumza na kupigiwa makofi na wananchi wakati akihamasisha ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Nyagisya wilayani humo, jana Jumamosi Januari 23, 2021. 

 

KUNA kila dalili kuwa zahanati ya kijiji cha Nyagisya wilayani Tarime, Mara itakamilika haraka na kuanza kutoa huduma za afya kwa wananchi kijijini.

 

Msukumo wa ujenzi wa zahanati hiyo umeshika kasi. Hali hiyo imedhihirika jana Jumamosi Januari 23, 2021 ambapo Mkuu wa Wilaya (DC), Mhandisi Mtemi Msafiri amezuru kijijini hapo na kuweka bayana mpango mkakati wa kuharakisha ujenzi huo.

 

“Kwanza hapa tayari kuna nguvu za wananchi, Mbunge wa [wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara] ametoa shilingi milioni tano kutoka Mfuko wa Jimbo na Halmashauri [ya wilaya] ilishetenga milioni 25 kwa ajili ya mradi huu,” amesema Mhandisi Msafiri.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon.

DC Msafiri amezuru eneo la ujenzi wa zahanati hiyo na kushuhudia baadhi ya vifaa vya ujenzi kama vile matofali, mawe na mchanga vilivyokwisha kuwasilishwa kwa ushirikiano wa wananchi na halmashauri ya wilaya.

 

Kuhusu taarifa za wajawazito kupata huduma ndani ya chumba cha darasa kijijini hapo, mkuu huyo wa wilaya amesema zahanati ya kijiji jirani cha Mtana imekuwa ikitoa huduma za kliniki ya wajawazito na watoto kijijini Nyagisya kwa njia ya mkoba (mobile clinic), ambapo wajawazito wamekuwa wakipatiwa huduma ndani ya ofisi ya serikali ya kijji hicho.

 

Kuhusu tuhuma kwamba muuguzi wa zahanati ya Mtana, Rebecca Messo kuhudumia wajawazito katika mazingira yasiyo rafiki, DC Msafiri amesema “Mkurugenzi [Mtendaji wa Halmashauri] atafuatilia sula hilo na kuchukua hatua kama kuna uzembe ulifanyika,” amesema.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya (DED) ya Tarime, Apoo Castro Tindwa amesema ofisi yake itashirikiana na wakazi wa kijiji cha Nyagisya kuharakisha mradi huo wa zahanati.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nyagisya wakiwa katika eneo la ujezi wa zahanati.

Ukosefu wa zahanati katika kijiji cha Nyagisya umekuwa ukisababisha wanakijiji kulazimika kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za afya.

 

Nao wakazi wa kijiji hicho wamewapongeza viongozi hao kutokana na ushirikiano wanaowapa katika mkakati wa kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages