NEWS

Wednesday 20 January 2021

Zimamoto Mara mguu sawa elimu ya kukabili majanga ya moto

Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Mrakibu Msaidizi Augustine Magere.

JESHI la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara limejipanga kuendelea kuelimisha wananchi na ofisi mbalimbali namna ya kukabiliana na majanga ya moto.

 

Jeshi hilo litatumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha wadau mbalimbali umuhimu wa kulipia maduhuri ya serikali kwa mujibu wa sheria.

 

Akizungumza na Mara Online News ofisini kwake jana Januari 19, 2021, Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Mrakibu Msaidizi Augustine Magere, amesema upo umuhimu mkubwa wa wananchi kufikishiwa elimu hiyo.

 

Magere amesema kwa kushirikiana na maofisa watendaji wa kata na wenyeviti wa serikali za mitaa, watatoa elimu kuhusiana na vitu vinavyoweza kusababisha moto na hatua za awali za kuchukua kabla ya kikosi hicho kufika eneo la tukio.

 

Amesema wananchi kwa sasa wanatumia gesi majumbani na kwamba bila kuwa na uelewa wa matumizi sahihi wanaweza kuzisababisha kulipuka moto na kuleta madhara makubwa.

 

Mrakibu Msaidizi huyo amesema pamoja na kutoa elimu juu ya viashiria vya moto, upo umuhimu wa wananchi kuwa na vifaa vya huduma ya kwanza ya kuzima moto majumbani ikiwemo mchanga.

Fire extinguishers ni miongoni mwa vifaa vya kukabiliana na majanga ya moto

“Ni jukumu letu kutoa elimu kama kikosi cha Zimamoto na tutaanza tena hivi karibuni kwa kuanzia kwa wananchi na baadaye katika maeneo ya masoko, migodi, ofisi za umma na watu binafsi.

 

“Huko kwa wananchi pia wapo watu ambao sio waaminifu, ambao wanahujumu miundombinu kwenye visima vya kutolea maji vilivyopo mitaani, tunataka tukazungumze nao maana huo ni uhujumu uchumi,” amesema Magere.

 

Amesema wafanyabiashara wanaendelea kukumbushwa kuwa na vifaa vya kuzimia moto na kulipia maduhuri ya serikali kwa mujibu wa Sheria Na. 14 ya Mwaka 2017 na Kanuni zake za Mwaka 2008, 2010, 2015 na 2020.

 

(Imeandikwa na Shomari Binda, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages