NEWS

Monday 8 March 2021

Afisa Madini Mara amaliza mgogoro wa wachimbaji wadogo Tarime

Afisa Madini wa Mkoa wa Mara, Nyaisara Mgaya (kushoto), akizungumza katika mkutano wa kutatua mgogoro baina ya wachimbaji wadogo wa mgodi wa dhahabu wa Marera uliopo Nyamongo wilayani Tarime.
 

AFISA Madini wa Mkoa wa Mara, Nyaisara Mgaya amefanikiwa kutatua kwa amani mgogoro baina ya wachimbaji wadogo katika mgodi wa dhahabu wa Marera uliopo kijiji cha Kerende, Nyamongo wilayani Tarime.

 

Mgaya amefanikiwa kutatua mgogoro huo leo Machi 8, 2021 na kuruhusu shughuli za uchimbaji kuendelea kwa kuzingatia maafikiano yaliyofikiwa katika mkutano wake na wamiliki wa mashimo husuka mgodini hapo.

Utatuzi wa mgogoro ukiendelea.

Mgogoro huo ambao ulisababisha Serikali kufunga uchimbaji kwenye mashimo yenye mgogoro kwa wiki tatu, ulikuwa ni kati ya Marwa Mroni na Mwita Makindya wenye leseni za kumiliki mashimo ya uchimbaji dhahabu katika mgodi huo wa Marera.

 

Katika mvutano huo, Mroni alilalamikiwa kuendesha shughuli za uchimbaji hadi kutobokezea kwenye eneo linalomilikiwa na Makindya.

Wachimbaji wagodo wakifuatilia utatuzi wa mgogoro huo.

Afisa Madini wa Mkoa, Mgaya, amechukua hatua ya kushughulikia mgogoro huo kitaalamu kwa kumleta mtaalamu wa upimgaji ambaye amebainisha kuwa ni kweli Mroni alivuka eneo lake la leseni na kuingilia miliki ya Makindya.

 

“Mpimaji amebaini kuwa shimo namba moja na namba mbili (yaliyopo kwenye leseni ya Mroni) yameingia mita 12 ndani ya eneo la mwingine, hivyo wanatakiwa kurudi waachie eneo hilo sasa liwe chini ya usimamizi wa Mwita Makindya,” amesema Mgaya na kupigiwa makofi na umati wa wachimbaji wadogo wa mgodi wa Marera.

Afisa wa Jeshi la Polisi akichangia mada wakati wa utatuzi wa mgogoro huo.
 

Mgaya ametumia nafasi hiyo pia kuhimiza suala la usalama na usafi wa mazingira katika mgodi huo kwa kuwataka wachimbaji wadogo kuchukua tahadhari ili kuepuka milipuko ya magongwa.

 

Kwa upande wao, Mroni na Makindya wamepokea tamko hilo la afisa madini kwa kukubali kuzingatia maelekezo ya kila mmoja kuchimba kwenye eneo lake la leseni.

 

Afisa Tarafa ya Ingwe ulipo mgodi wa Marera, James Yunge amemshukuru afisa madini huyo na wachimbaji hao kwa kumaliza mgogoro huo kwa amani na kuwataka wasianzishe migogoro mingine.

 

Aidha, Yunge amewataka wachimbaji hao kuepuka kosa la kutorosha dhahabu kwenda nchi jirani ila wahakikishe wanaiuza kwenye masoko maalumu yaliyoanzishwa na Serikali.

Afisa Tarafa ya Ingwe ulipo mgodi wa Marera, James Yunge (wa pili kulia), akisisitiza jambo katika mkutano huo.

Pia wachimbaji hao wamewahimizwa kulipatia suala la usalama kipaumbele, kupendana na kushirikiana katika uendeshaji wa shughuli hizo.

 

Katika hatua nyingine, Afisa Madini wa Mkoa, Mgaya, amewashauri wachimbaji wadogo wa mgodi huo kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ili kuwawezesha kufanya uzalishaji wenye tija bila kuathiri mazingira.

 

“Mgodi huu ni potential [akimaanisha una dhahabu nyingi], wekezeni katika teknolojia kwa kuwa na miundombinu na vifaa vya kisasa,” Mgaya amewaambia wachimbaji hao.

Sehemu ya eneo la mgodi wa dhahabu wa Marera.

Mgodi huo wa Marera unatajwa kuwa miongoni mwa migodi inayozalisha kiwango kikubwa cha dhahabu katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime.

 

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages