NEWS

Tuesday 9 March 2021

ATFGM Masanga yakutanisha Kenya na Tanzania mapambano ya ukeketaji, DAS Tarime ataka elimu ianzie shuleni

Wadau wa mapambano dhidi ya ukeketaji na ndoa za utotoni wakishiriki warsha iliyoandaliwa na Shirika la ATFGM Masanga mjini Tarime, leo.

KATIBU Tawala wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, John Marwa ameshauri elimu kuhusu ukeketaji iwe sehemu ya masomo katika shule za msingi na kuendelea ili kuwezesha wanafunzi kufahamu madhara ya ukatili huo wa kijinsia.

 

“Elimu ya ukeketaji itolewe kuanzia shule za msingi, wanafunzi waelezwe madhara ya ukeketaji na namna ya kupambana nao,” amesesitiza Marwa katika hotuba yake ya ufunguzi wa warsha ya kujadili ukeketaji na madhara yake katika maeneo ya mpakani upande wa Tanzania na Kenya.

Katibu Tawala Wilaya ya Tarime, John Marwa (aliyesimama) akifungua warsha hiyo. Kulia waliokaa ni Mkurugenzi wa Shrika la ATFGM Masanga, Sista Bibiane Bokamba na wengine ni viongozi mbalimbali.
 

Warsha hiyo ya siku moja imeandaliwa na kuratibiwa na Shirika lisilo la Serikali la ATFGM Masanga na kufanyika leo Machi 9, 2021 mjini Tarime kwa kushirikisha wadau zaidi ya 50 wakiwemo viongozi wa wilaya, jeshi la polisi, halmashauri, tarafa, dawati la jinsia, idara za ustawi na maendeleo ya jamii.

 

“Tushirikiane kutoa elimu ya kupiga vita mila ya ukeketaji na kuchukua hatua dhidi ya wanaoikumbatia. Lakini pia tukazanie elimu kwa watoto wetu wa kike kwani ndiyo msingi wa maisha bora duniani,” ameongeza Marwa ambaye amemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Tarime katika warsha hiyo.

 

Aidha, Katabu Tawala huyo ametumia nafasi hiyo kukemea akina mama wanaohamasisha ukeketaji kwa watoto wa kike badala ya kuwa mstari wa mbele katika kupinga ukatili huo wa kijinsia.

Meneja wa Shirika la ATFGM Masanga, Valerian Mgani (kulia) na baadhi ya washiriki wengine wa warsha hiyo.
 

Halmashauri ya Wilaya ya Tarime chini ya muongozo wizara yenye dhamana ya afya inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kupambana na mila na desturi zenye madhara katika jamii ukiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni.

 

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Tarime, Ramadhani Sarige amesema baadhi ya wasichana hulazimishwa kukeketwa na kwamba mtoto aliyekeketwa anastahili kuhurumiwa na kupewa msaada wa kutibiwa majeraha badala ya kumshtaki kwa kosa hilo.

 

Akielezea hali ya ukeketaji kwa upande wa Kenya, Mwakilishi wa Tarafa ya Ntimaru, Mwita Joseph Chacha amesema Rais Uhuru Kenyata ameshatangaza kuwa ukeketaji unatakiwa kutokomezwa nchini humo kufikia mwaka 2022.

 

“Ukeketaji una madhara makubwa kwa watoto wa kike na jamii, sisi Kenya tumeungana kuanzia ngazi ya kijiji kupambana na tatizo hili kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali,” amesema Chacha.

Sehemu ya washiriki wa warsha hiyo.

Chacha ameongeza kuwa nchini Kenya mtu anayepata taarifa za ukeketaji na kukaa kimya bila kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola huchukuliwa kuwa ametenda kosa la jinai na anapobainika hushtakiwa mahakamani.

 

Amebainisha kwamba makabila yanayotekeleza mila ya ukeketaji yaishi mpakani mwa Tanzania na Kenya, hivyo juhudi za pamoja zitasaidia kupunguza ukeketaji katika maeneo hayo.

 

Ili kuongeza ufanisha katika mapambano dhidi ya ukeketaji na ndoa za utotoni, Chacha ameshauri wanawake waliokeketwa washirikishwe kutoa elimu kuhusu madhara ya vitendo hivyo vya ukatili.

 

Amesema warsha hiyo itawezesha wadau kutoka pande zote mbili (Tanzania na Kenya) kupeana uzoefu na mbinu za kupambana na vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni.

 

Naye Mkurugenzi wa Shirika la ATFGM Masanga, Sista Bibiana Bokamba amesema ushirikiano wa wadau kutoka maeneo ya mpakani utasaidia kupunguza vitendo hivyo kwani baadhi ya ngariba (wakeketaji) na watoto waliokeketwa wamekuwa wakkimbilia upande wa pili kukwepa mkono wa sheria.

Washiriki wengine ya wakifuatilia mada katika warsha hiyo.

Awali, Meneja wa Shirika la ATFGM Masanga, Valerian Mgani amesema warsha hiyo ni mwendeleo wa nyingine kadhaa zilizokwishafanyika kwa lengo la kujadili na kuweka mipango ya kupambana na vitendo vya ukeletaji na ndoa za utotoni katika jamii.

 

Shirika la ATFGM Masanga lenye makao makuu katika kijiji cha Masanga wilayani Tarime limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kuanzisha kambi okozi kwa ajili ya watoto wanaokimbia mashinikizo ya kukeketwa na ndoa za utotoni.

 

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages