NEWS

Monday 8 March 2021

‘Wajanja’ wahujumu mradi wa elimu Tarime Vijijini

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijiji), Apoo Castro Tindwa.

SARUJI iliyokuwa imenunuliwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na choo katika Shule ya Msingi Weigita iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) imehujumiwa.

 

“Tunashangaa walioiba saruji mifuko 68 wamekamatwa wakaachiwa na hakuna chochote kinachoendelea, huku wananchi tunaambiwa tutoe michango, waananchi tunaumia sana," amesema mtoa taarifa wetu kutoka kijijini Wegita, juzi.

 

Mwananchi huyo amesema kijiji hicho kilipokea Sh milioni 68 kutoka Halmashauri hiyo kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na choo katika shule hiyo.

 

Ameongeza kuwa mbali na wizi wa saruji hiyo, wanatilia shaka ubora wa kazi iliyofanyika shuleni hapo.

 

"Hiyo pesa tuliambiwa imetoka TAMISEMI lakini imejenga madarasa mawili bila usimamizi wa mhandisi na pesa imeisha choo hakijajengwa," amedai mwanakijiji huyo.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijiji), Apoo Castro Tindwa ameulizwa na Mara Online News akakiri kutokea kwa wizi wa saruji hiyo.

 

“Ni kweli wizi wa saruji mifuko 68 umebainika katika Shule ya Msingi Weigita na watuhumia wote wamefikishwa polisi na kupewa dhamana kwa sharti la kurejesha saruji hiyo," amesema Tindwa.

 

Kuhusu ubora wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa bila usimamizi wa utaalamu, Tindwa ameahidi kumtuma mhandisi wa halmashauri hiyo kwenda kukagua kazi iliyofanyika.

 

Pamoja na vyanzo vingine vya ndani, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) inapata mapato makubwa kutokana na uwepo wa mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo.

 

Hivi karibuni, mgodi huo uliikabidhi halmashauri hiyo hundi ya Sh zaidi ya bilioni mbili ikiwa ni ushuru wa huduma katika kipindi cha miezi sita iliyoisbia Juni 2020.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages