NEWS

Wednesday 24 March 2021

Baada ya kuchimba vyoo, wachimbaji mgodi wa Marera waelimishwe faida za kuvitumia

Wachimbaji wadogo wa mgodi wa dhahabu wa Marera wakipokea maelekezo mbalimbali yakiwemo ya kuchimba vyoo.

HIVI karibuni, wachimbaji wadogo wa mgodi wa dhahabu wa Marera uliopo kwenye bonde la mto Mara katika wilaya ya Tarime mkoani Mara - Tanzania, waliagizwa na mamlaka za serikali kuchimba vyoo kwa ajili ya matumizi yao na wauzaji wa vyakula mgodini hapo.

 

Mgodi huo umekuwa ukiendeshwa bila vyoo tangu ulipoanzishwa miaka kadhaa iliyopita na unategemewa na mamia ya wachimbaji wadogo kwa ajili ya kujipatia kipato cha kuwawezesha kumudu mahitaji yao na familia zao.

 

Agizo hilo lilitolewa na Afisa Tarafa ya Ingwe ulipo mgodi wa Marera, James Yunge baada ya kutembelea huko na kubaini kuwa wachimbaji hao wanajisaidia haja kubwa na ndogo vichakani kutokana na ukosefu wa vyoo katika eneo hilo.

 

Hatua hiyo inalenga kuepusha athari za kiafya kwa binadamu na uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya mgodi wa Marera na bonde la mto Mara kwa ujumla.

 

Waliopewa jukumu la kuchimba vyoo ni wamiliki wa mashimo ya uchimbaji wa dhahabu kwa ajili ya matumizi yao, wafanyakazi wao na wafanyabiashara wakiwamo wauzaji wa vyakula na vinywaji.

 

Kwa mujibu wa mtaalamu wa afya msaafu, Dkt Omchamba Salimba, athari za vitendo vya watu kujisaidia vichakani ni pamoja na kusababisha harufu mbaya, mlipuko wa magonjwa ya kipindupindu, kuhara na yale yanayosababishwa na minyoo kama vile upungufu wa damu na utapiamlo kwa watoto.

 

Naye Dkt John Chacha wa Kituo cha Afya cha Makongoro, anataja athari nyingine za vitendo vya watu kujisaidia vichakani kuwa ni kusomba vinyesi kwenda kwenye vyanzo vya maji wakati wa mvua.

 

“Migodi mingi ya madini iko maeneo ya vilima na mwinuko, hivyo kama wachimbaji wanajisaidia vichakani ni rahisi vinyesi vyao kusombwa kwenda mitoni na kuhatarisha watumiaji wa maji hayo,” anasema Dkt Chacha.

 

Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini Wilaya ya Tarime, Kitunka Nyirabu anasema baada ya agizo la kuchimba vyoo katika mgodi wa Marera, ameanza ziara ya kutembelea migodi mingine wilayani humo kuhamasisha wachimbaji wadogo kuchimba vyoo.

 

“Nimeanza ratiba ya kutembelea migoni mingine ndani ya wilaya kuhamasisha suala hili na tayari baadhi ya migodi ukiwemo wa Gamasara imeanza kuchimba vyoo,” anasema Nyirabu.

 

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kuna migodi ya wachimbaji wadogo wa madini zaidi ya 30 wilayani Tarime inayohudumia wastani wa wachimbaji 3,000 kwa siku.

 

Anakiri kwamba migodi mingi kati ya hiyo wachimbaji wake wamekuwa wakijisaidia vichakani kutokana na ukosefu wa vyoo.

Sehemu ya bonde la mto Mara, sio mbali sana na ulipo mgodi wa Marera. 
 

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kerende ulipo mgodi huo, Mniko Magabe, anasema kwa sasa suala la kuchimba vyoo mgodini hapo ni la lazima.

 

Naye Afisa Madini wa Mkoa wa Mara, Nyaisara Mgaya anaungana na viongozi hao kuwahimiza wachimbaji hao kutekeleza agizo hilo akisema suala la uchimbaji wa vyoo ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika migodi ya madini.

 

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kemambo ulipo mgodi wa Marera, Paul Maisori, ameelekeza utekelezaji uchimbaji vyoo utekelezwe sambamba na kuwatengea wauza vyakula na vinywaji eneo maalumu - tofauti na mtindo wa kila mmoja kujichagulia aneo la kuendeshea biashara yake mgodini hapo.

 

Wachimbaji wadogo wenye leseni katika mgodi huo wakiwamo Mwita Makindya na Marwa Mroni wanasema wako tayari kutekeleza agizo la kuchimba vyoo mgoni hapo.

 

Kimsingi ni jambo jema kuchimba vyoo na hata kutenga eneo maalumu la wauza vyakula na vinywaji katika migodi ya wachimbaji wadogo wa madini ukiwemo wa Marera kwa ajili ya kuepusha madhara ya kiafya na kimazingira.

 

Hata hivyo, pamoja na hatua hiyo muhimu, kuna haja sasa ya mamlaka husika kupeleka elimu ya afya na kuhusu matumizi sahihi na bora ya vyoo.

 

Elimu hiyo itasaidia kubadilisha tabia za wachimbaji hao ambao walizoea kujisaidia vichakani kwa miaka mingi ili sasa wajue umuhimu wa kujisaidia vyooni na faida zake, na kwa upande mwingine, wafahamu athari za kujisaidia vichakani, namna ya kuziepuka na kukabiliana nazo.

 

Ninasema hivyo kwa sababu suala la kuchimba vyoo na matumizi ya vyoo ni vitu viwili tofauti, hivyo mamlaka za serikali zitakuwa hazijawasaidia ipasavyo wachimbaji hao ikiwa zitaishia kuwahamasisha kuchimba vyoo bila kuwapatia elimu ya matumizi sahihi na bora ya vyoo hivyo.

 

Hii ni sawa na kusema kwamba unaweza kuchimba vyoo lakini wachimbaji hao wakapuuza kuvitumia na kuendelea kujisaidia vichakani kutokana na kutojua umuhimu na matumizi sahihi na bora ya miundombinu hiyo.

 

Kwa mantiki hiyo, kama ambavyo mamlaka za serikali zimeona ni muhimu wa kuhamasisha na kuagiza ujenzi wa vyoo katika mgodi wa Marera na mingineyo, zione pia umuhimu wa kuwapelekea wachimbaji wadogo elimu ya kuwawezesha kujua umuhimu na faida za matumizi sahihi na bora ya vyoo.

 

(Uchambuzi na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages