NEWS

Saturday 27 March 2021

Kupanda miti sawa, pia tuepuke uchafuzi Bonde la Mto Mara

Ukataji wa miti kama huu unachangia uchafuzi wa maji katika mto Mara

HIVI karibuni wananchi wanaoshi maeneo ya bonde la mto Mara na mto Mori katika wilaya ya Tarime na Rorya, Mara - Tanzania wameadhimisha Wiki ya Maji kwa kupanda miti kwenye maeneo ya hifadhi za vyanzo vya maji.

 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji ukanda wa Mara Kaskazini, Siproza Charles ameiambia Mara Online News kwamba wamefanya hivyo kwa lengo la kutunda uendelevu wa vyanzo vya maji na mazingira.

 

Siproza amesema wamelenga kupanda miti 6,000 katika vijiji vya Nkerege, Mara Sibora na Kwibuse - sawa na miti 2,000 kila kijiji.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Bonde la Mto Mori, Thomas Nkaina, amesema mbali na kupanda miti wataendelea kuelimisha wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.

 

Maadhimisho ya Wiki ya Maji nchini yamefanyika kuanzia Machi 16 na kuhitimishwa Machi 22, 2021- yakiwa na kaulimbiu inayosema “Thamani ya Maji kwa Uhai na Maendeleo.”

 

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) ni mdau mkubwa wa kuwezesha jumuiya hizo za watumia maji kutekeleza wajibu wao wa kulinda na kuhifadhi mto Mara na mto Mori.

 

Mito hiyo ambayo inatiririsha maji kwenye Ziwa Victoria ni mito muhimu kwa ustawi wa ziwa hilo, maisha ya wananchi na viumbe hai wengine.

 

Mfano, mto Mara unawezesha uwepo wa mamia ya nyumbu wanaohama kila mwaka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

 

Afisa Maji Dakio la Mara-Mori, Mhandisi Mwita Mataro amesema upandaji wa miti katika maenea vyanzo vya maji umepewa kipaumbele katika maadhimisho ya Wiki ya Maji mwaka huu.

 

Amesema hivi karibuni ofisi yake imepanda miti 16,000 katika maeneo yaliyo jirani na mto Mara upande wa wilaya za Serengeti na Butiama mkoani Mara.

 

Kimsingi suala la kupanda miti lina umuhimu mkubwa kwa uendelevu wa vyanzo vya maji, lakini kwa upande mwingine wananchi wanaoishi katika maeneo ya bonde la mto Mara na mto Mori pia wana jukumu la kuepuka uchafuzi wa maji na ardhi kutokana na shughuli za binadamu.

Kilimo na ufugaji ni miongoni mwa shughuli za binadamu zinazofanyika katika bonde la mto Mara
 

Mtaalamu wa Maji kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) linalojumuisha bonde la mto Mara na mto Mori, Ogoma Mangasa anasema kumekuwepo uchafunzi wa maji na uharibifu wa ardhi kutokana na shughuli za binadamu kama vile ufugaji, kilimo, uchimbaji madini, matumizi ya zebaki, ukataji miti ovyo na uchomaji moto zinazotishia ubora na uendelevu wa rasilimali za maji.

 

Majukumu ya LVBWB ni kusimamia na kuratibu matumizi bora ya maji, kutoa vibali vya kutumia maji na kutupa maji taka, kukusanya ada ya matumizi ya maji na kutatua migogoro ya matumizi ya rasilimali hiyo.

 

Pia kudhibiti, kuchukua hatua dhidi ya wachafuzi wa maji na vyanzo vyake, kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji, kuangalia ubora na usafi wa maji na kufanya utafiti wa maji ardhini.

 

Bonde la Ziwa Victoria ni eneo ambalo mwelekeo wa maji yake hatimaye huingia katika ziwa hilo. Mikoa iliyopo kwenye bonde hilo kwa upande wa Tanzania ni Mwanza, Kagera, Mara, Simiyu, Geita na Shinyanga.

 

Shughuli za kiuchumi na kijamii zinazohitaji maji katika bonde hilo ni matumizi ya nyumbani na mifugo, kilimo cha umwagiliaji, viwanda, migodi ya madini, biashara, usafiri na usafirishaji, utalii, uvuvi na ufuaji umeme.

 

Mwelimishaji jamii juu ya usimamizi wa rasilimali za maji, Godfrey Mkungu kutoka LVBWB, anasema sheria na sera za maji zimetungwa kwa kuzingatia umuhimu wa maji kwa viumbe hai.

 

“Bila maji hakuna uhai. Aidha, maji ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kiwango cha maendeleo ya jamii yoyote kinategemea uwepo wa maji ya kutosha na yenye ubora unaotakiwa.

 

“Katika hali yake ya asili, maji ni sehemu ya mazingira ambapo wingi na ubora wake ndio husaidia katika kuamua jinsi yatakavyotumika,” anasema Mkungu.

 

{Makala: Christopher Gamaina - Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages