NEWS

Thursday 25 March 2021

Mbunge Mathayo: Wapuuzeni wanaonizushia kifo

Mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo Manyinyi

 

MBUNGE wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo Manyinyi amewataka wananchi kuwapuuza wanaomzushia kifo kwa kuwa anayo afya njema.

 

Akizungumza na Mara Online News mjini Musoma leo, Mathayo amesema waliosambaza taarifa hizo wana nia ovu ya kuzusha taharuki kwa wananchi kipindi hiki cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt John Pombe Magufuli.

 

Mbunge huyo amewaondoa hofu wananchi wa jimbo hilo na Watanzania kwa ujumla na kuwaendelea kuwa watulivu, kudumisha upendo, umoja na amani.

 

“Niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Musoma Mjini kutokana na taarifa ambazo siyo za kweli ambazo zimekuwa zikizungumzwa huko mitaani.

 

“Mimi mbunge wao nipo salama na mwenye afya njema na tuko pamoja katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wetu Hayati Dkt John Pombe Magufuli,” amesema Mathayo.

 

Akizungumzia kifo cha Rais Magufuli, amesema ni msiba mkubwa katika Taifa, hivo wananchi wanatakiwa kusimama imara katika kipindi hiki cha maombolezo.

 

Mathayo amewaomba wananchi wa Musoma Mjini na Watanzania wote kuendelea kumuombea dua Hayati Dkt Magufuli ili apumzuke kwa amani katika nyumba yake ya milele.

 

(Habari: Shomari Binda, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages