NEWS

Monday 1 March 2021

Madiwani Tarime Mji mafunzoni

 

Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime (DAS) John Marwa akifungua mafunzo ya Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime  leo  asubuhi katika chuo cha Tarime nursing school, Kushoto ni  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa, na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri  ya mji wa Tarime, Daniel Komote na makamu wake Thobias Ghati.

Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Mkoani Mara leo Machi 1,2021 wameanza  kupata mafunzo  yanayolenga kuwawezesha  kutekeleza wajibu  wao  kwa ufanisi.

Mafunzo  hayo  yatahusisha mada 18 zikiwemo, uongozi na utawala bora, sheria za uendeshaji wa Serikali za mitaa, muundo, madaraka na majukumu ya Serikali za mitaa,  maadili  ya utumishi wa umma, uibuaji na utekelezaji wa miradi ya kijamii.

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime wakishiriki katika mafunzo  hayo
Akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa chuo cha wauguzi Tarime leo asubuhi Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime (DAS) John Marwa amesema mafunzo hayo  yatawawezesha madiwani hao  kutekeleza  majukumu yao kwa kasi na viwango vinavyotakiwa.

“Naipongeza sana Halmashauri ya Mji Tarime kwa kuona umuhimu wa kuendesha  mafunzo  haya kwa madiwani. Hii ni Shule tosha  na baada ya mafunzo hayo Halmashauri na iwe bora na yenye kasi kubwa ya kuwaletea wananchi wetu maendeleo’, DAS Marwa ambaye amefungua mafunzo hayo  kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime (DC) Mhandisi Mtemi Msafiri  amesema.

 Mkurugenzi wa Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa  amesema mafunzo hayo  yatadumu kwa siku tatu mfululizo.

“ Lengo ni kuwajengea uwezo madiwani wetu  kuna mada 18 katika mafunzo haya na yanahusisha pia Wabunge wetu  “, amesema Ntiruhungwa .

Mkurugenzi wa Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa akitoa maelezo  kuhusu  mafunzo  hayo. 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote  amewataka madiwani wenzake kushiriki kikamilifu  katika mafunzo hayo. Mafunzo hayo yanatolewa na wakufunzi kutoka Chuo cha Serikali za mitaa cha Hombolo kilichopo Dodoma na yanahusisha Wabunge ambao ni sehemu ya madiwani wa Tarime Mji.

“ Mafunzo hayo yana faida kubwa kwa Halmashauri yetu na wananchi wetu”, amesema Komote ambaye  ni diwani wa kata ya Nkende kupitia chama tawala (CCM).

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote akisisitiza  umuhimu wa mafunzo hayo

CCM ilishinda viti vyote vya udiwani  katika jimbo  la Tarime katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages