
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (aliyevaa suti), akikagua Mgodi wa Dhahabu wa Kinyambwiga wilayani Bunda jana.
Bunda
----------
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewataka wachimbaji wa madini kufanya kazi kwa bidii, huku wakizingatia masuala ya afya, usalama na ustawi wao kazini.
RC Mtambi aliyasema hayo Jumatatu, Desemba 15, 2025 alipokwenda kukagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa katika Mgodi wa Dhahabu wa Kinyambwiga uliopo wilayani Bunda.
Alieleza kuridhishwa na utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya Machi 2025, ikiwemo upatikanaji wa umeme, maji, ulinzi na barabara, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 90.
Alipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mara, TANESCO, TANROADS, Mkurugenzi wa Halmashauri na Mkuu wa Wilaya ya Bunda pamoja na Serikali ya Mtaa husika kwa juhudi kubwa zilizofanyika katika kurahisisha shughuli za uchimbaji mgodini hapo.
Vilevile, RC Mtambi alikagua maendeleo ya mgodi huo kwa ujumla na kupongeza uongozi husika kwa hatua zilizofikiwa, hususan katika maeneo ya miundombinu na mazingira ya ufanyaji kazi, akieleza kuridhishwa na maboresho yanayoendelea kufanyika.

RC Mtambi alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa sekta ya madini katika kukuza uchumi wa taifa, hususan kupitia wachimbaji wadogo na wawekezaji.
Hivyo, kiongozi huyo wa mkoa aliwataka wachimbaji wadogo wadogo kuendelea kufanya kazi kwa utu, bidii, weredi na ubora, akisisitiza kuwa ataendelea kuwa mlezi wao kama alivyoahidi awali.
Sambamba na hayo, RC Mtambi alisikiliza kero mbalimbali za wananchi wa kata ya Kinyambwiga, zikiwemo changamoto za miundombinu ya shule na huduma za afya.
Baadaye aliwaagiza viongozi wa mamlaka husika, akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kushughulikia kero hizo kwa wakati ili kuboresha huduma za jamii na kuwezesha wananchi hao kuendelea na shughuli za uzalishaji kwa ufanisi zaidi.
No comments:
Post a Comment