NEWS

Tuesday 30 March 2021

Rais Samia amteua Dkt Mpango kuwa Makamu wake, Bunge labariki

Makamu wa Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Mpango.
 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemteua Dkt Philip Mpango ambaye baadaye amethibitishwa na Bunge kwa asilimia 100 (wabunge wote 363 wamempigia kura za ndiyo) leo Jumanne Machi 30, 2021 kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Rais Samia amefanya uteuzi huo kwa mamlaka ya kikatiba aliyonayo - chini ya Ibara ya 35 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
 

Kabla ya uteuzi huo, Dkt Mpango alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango - nafasi aliyoitumikia kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

 

Akizungumza baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kumpatia nafasi kabla ya kuthibitishwa, Dkt Mpango amemshukuru Mungu, Rais Samia na chama chake - tawala cha CCM kumwezesha kufikia hatua hiyo huku akisema "Nimepigwa na butwaa."

 

"Mimi huwa ninaamini kwamba kazi zote njema ni kazi za Mungu, kwa hiyo tunawajibika kufanya kazi njema kwa uwezo na nguvu zetu zote," amesema Dkt Mpango na kuongeza:

 

"Tumuenzi Dkt Magufuli [aliyekuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt John Pombe Magufuli] kwa kuishi ndoto yake ya kusimamia rasilimali za nchi na maadili ya utumishi wa umma... lazima tutende wajibu wetu kwa umma. Nawaahidi kuendelea kusimamia haki za wanyonge kwa uwezo wangu wote."

 

Aidha, Dkt Mpango ameongeza "Kwa watu wanaokula rushwa mimi siyo mpole... nawambieni ukweli nitamsaidia Rais kuhakikisha kwamba tunakwenda sawasawa. Kwa wale wanaodokoa rasilimali za nchi hao ni halali yangu, nitamsaidia Rais kwa manufaa ya Watanzania."

 

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipopewa nafasi amesema uteuzi huo wa Dkt Mpango ni chagua la Mungu na kumuelezea Makamu wa Rais huyo mpya kuwa ni mtu sahihi na mwenye uwezo mkubwa wa kuchapa kazi za dhamana aliyokabidhiwa.

"Namshukuru Rais [Samia Suluhu Hassan] kwa maono na utashi wa kumteua [Dkt Mpango]... tumpe ushirikiano," amesema Waziri Lukuvi.

 

#MaraOnlineNews-Update

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages