Baadhi ya wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari ya Kwibuse |
WANAFUNZI wa kike katika Shule ya Sekondari ya Kwibuse na wananchi wa kijiji ilipo shule hiyo wilayani Rorya, Mara - Tanzania, wanasubiri kwa shauku kubwa ujenzi wa choo cha wanafunzi hao.
Choo hicho kinatarajiwa kujengwa shuleni hapo chini ya mpango wezeshi wa Shirika la MWEA (Mara Women Empowerment Assistance) kupitia Kamati ya Maendeleo ya Serikali ya Kijiji cha Kwibuse.
Ofisa Mhamasishaji wa vikundi vinavyowezeshwa na MWEA, Msamba Chacha ameiambia Mara Online News jana Machi 28, 2021 kwamba ujenzi wa choo hicho utaanza baada ya wajumbe wa kamati hiyo kupatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kusimamia uendelevu wa mradi huo.
“Walituomba msaada wa kuwajengea choo chenye matundu sita kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule hiyo, lakini kabla ya kuanza kutekeleza mradi huo tutawapatia mafunzo maalum kupitia Shirika la OIKOS,” amesema Chacha na kufafanua:
“Mafunzo hayo yanalenga kuwafanya wajumbe wa kamati hiyo na wanakijiji kwa ujumla kuuona na kuuthamini mradi huo kama mali yao ili hata ukichakaa wawajibike kuukarabati.”
Wanafunzi walengwa wa mradi huo wanasema utawaondolea adha ya kutembea umbali wa mita 110 kwenda kujisaidia, hali inayowasababisha kupitwa na sehemu ya vipindi vya masomo darasani - tatizo ambalo haliwagusi wanafunzi wa kiume kwani wao wamejengewa choo jirani na majengo ya shule hiyo.
“Choo tunachotumia kwa sasa kiko mbali na majengo ya shule yetu, tunatumia hadi dakika 15 kutembea (kwa miguu) kwenda kujisaidia. Ukibanwa haja wakati wa mvua unalazimika kwenda unanyeshewa,” anasema Neema James, mwanafunzi wa kidato cha pili shuleni hapo.
Mwanafunzi mwingine wa kidato hicho, Flora Ntondo anasema “Choo chetu kiko mbali, tunatumia dakika nyingi kwenda kujisaidia, wakati mwingine ukirudi darasani unakuta mwalimu amefundisha mambo yamekupita. Lakini pia choo kipo katika mazingira ya vichaka yanayotuweka katika hatari ya kuumwa na nyoka.”
Kwa upande wake, Ghati Hamis ambaye pia anasoma kidato cha pili shuleni hapo, analishukuru Shirika la MWEA kukubali kuwajengea choo kipya - akisema “Tunafurahi kusikia taarifa za mpango wa kutujengea choo jirani na shule, tunaomba watuwekee pia miundombinu ya maji kukidhi mahitaji yetu.”
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kwibuse wakitoka eneo la choo wanachotumia (kinachoonekana kwa mbali nyuma yao) |
Taarifa zaidi kutoka shuleni hapo zinaeleza kuwa wakati mwingine baadhi ya wasichana wamekuwa wakijisaidia kwenye vichaka vilivyo jirani kutokana na uvivu wa kutembea kwenda kujisaidia katika choo hicho.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Kwibuse, Venus Chiguma anasema shule hiyo ina wanafunzi wa kike 72 wa kidato cha kwanza hadi cha tatu akifafanua kuwa wa kidato cha kwanza ni 25, cha pili 38 na cha tatu tisa.
Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Serikali ya Kijiji cha Kwibuse ambaye hakupenda kutajwa jina kwenye habari hii anasema choo kinachotumiwa na wanafunzi hao kipo katika eneo ambalo awali lilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo kabla ya mabadiliko ya kuijenga kwingine.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, James Maseke anasema wanakijiji wamejipanga kulipatia Shirika la MWEA ushirikiano wa dhati katika ujenzi wa choo kipya cha wanafunzi wa kike shuleni hapo.
“Kiukweli wananchi wa kijiji cha Kwibuse tunalishukuru Shirika la MWEA kukubali kutujengea mradi huo kwa sababu hatua hiyo itatupunguzia mzigo wa kuchangia shughuli za maendeleo,” anaongeza Maseke.
Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la HakiElimu Tanzania, mazingira bora ya vyoo yana mchango mkubwa katika maendeleo ya kitaaluma kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
(Habari: Christopher Gamaina, Rorya)
No comments:
Post a Comment