NEWS

Friday 19 March 2021

Rais Samia: Ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini

Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (kushoto mbele) akikagua gwaride maalum la kijeshi baada ya kuapishwa Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam, leo.

RAIS mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kusimama pamoja, kushikamana na kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini katika kipindi hiki cha maombolezo ya kifo cha mtangulizi wake, Rais Dkt John Pombe Magufuli kilichotokea Machi 14, 2021.

 

“Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini, si wakati wa kutazama yaliyopita bali ni wakati wa kutazama yajayo,” amesisitiza Rais Samia kwenye hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa kushika madaraka hayo, leo Machi 19, 2021 katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.

Samia Suluhu Hassan akiapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Samia ameongeza “Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama taifa, ni wakati wa kufarijiana, kuoneshana upendo, udugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu na utanzania wetu.”

 

Amesema kipindi hiki si cha kunyoosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele, kufutana machozi na kufarijiana na kuunganisha nguvu kwa ajili ya kuijenga Tanzania mpya ambayo Rais Magufuli aliitamani.


Samia Suluhu Hassan (kushoto) akiapishwa kuwa Rais wa Jamhuti ya Muungano wa Tanzania.

“Ni wakati wa kuomboleza na kutazama yale yote mema aliyotutendea, zaidi tuungane sote kumwombea [Dkr Magufuli] kwa Mwenyezi Mungu ampunzishe kwa amani mahali pema peponi, amina,” ameongeza kiongozi huyo wa nchi.

 

Aidha, Rais Samia amewahakikishia Watanzania kuwa Taifa liko imara, viongozi wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaendeleza pale alipoishia Rais Magufuli na kwamba hakuna jambo litakaloharibika.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages