NEWS

Tuesday 23 March 2021

Rais Samia: Tuungane kuijenga Tanzania aliyoitamani Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia umma baada ya kuapishwa.

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaomba Watanzania kuunganisha nguvu za kuijenga Tanzania mpya ambayo mtangulizi wake, Rais Dkt John Pombe Magufuli aliitamani.

 

Rais Samia ametoa wito huo Ikulu - Magogoni jijini Dar es Salaam Machi 19, 2021, katika hotuba yake ya kwanza kwa Watanzania, baada ya kuapishwa kuwa Rais kuziba nafasi hiyo iliyoachwa na Dkt Magufuli aliyefariki dunia.

Rais Samia akila kiapo cha urais.
 

“Sote tunafahamu Magufuli alivyoipenda nchi hii na alivyojitoa kuwatumikia watu wake. Sote tulishuhudia kiu, dhamira na nia yake njema na ya dhati ya kutaka kuibadili nchi yetu na kuipatia mafanikio makubwa.

 

“Sote ni mashahidi wa namna ambavyo ameweza kuibadili taswira ya nchi kwa vitendo na kwa utendaji wake imara usiotikitisika wala kuyumbishwa huku muda wote akimtanguliza mungu mbele.

 

“Sote tulisikia matamanio na maono yake makubwa kwa nchi hii yaliyotafsiri katika mipango mikakati na ujenzi wa miradi mikubwa,” amesema Rais Samia.

 

Ameendelea kuwahimiza wananchi kushikamana na kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini katika kipindi hiki cha maombolezo ya kifo cha Rais Magufuli.

 

“Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini, si wakati wa kutazama yaliyopita bali ni wakati wa kutazama yajayo,” alisisitiza mkuu huyo wa nchi.

 

Ameongeza “Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama taifa, ni wakati wa kufarijiana, kuoneshana upendo, udugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu na utanzania wetu.”

 

Rais Samia ameongeza kuwa kipindi hiki si cha kunyoosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele, kufutana machozi na kufarijiana na kuunganisha nguvu kwa ajili ya kuijenga Tanzania mpya ambayo Rais Magufuli aliitamani.

 

“Ni wakati wa kuomboleza na kutazama yale yote mema aliyotutendea, zaidi tuungane sote kumwombea [Dkr Magufuli] kwa Mwenyezi Mungu ampunzishe kwa amani mahali pema peponi, amina,” ameongeza.

 

Rais huyo amewahakikishia Watanzania kuwa Taifa liko imara, viongozi wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaendeleza pale alipoishia Rais Magufuli na kwamba hakuna jambo litakaloharibika.

 

“Isitoshe nchi yetu inayo hazina nzuri ya viongozi na misingi imara ya utaifa, udugu, umoja na ustahimilivu, na nidhamu ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama iliyojengwa na viongozi waliotutangulia kwa kuanzia waasisi wetu, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee wetu Abeid Amani Karume. Niwahakikishie kuwa hakuna jambo litakaloharibika.

 

“Mimi nilipata bahati ya kuwa Makamu wake [wa Rais Magufuli], alikuwa ni kiongozi asiyechoka kufundisha, kuelekeza kwa vitendo jinsi anataka nchi hii iwe au nini kifanyike, Amenifundisha mengi, amenilea na kuniandaa vya kutosha, naweza kusema bila chembe ya shaka kuwa tumepoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mzalendo, mwenye maono, mpenda maendeleo, mwana mwema wa bara la Afrika na mwanamapinduzi wa kweli.

 

“Mheshimiwa Magufuli alikuwa chachu ya mabadiliko, kwa kweli tumepelea kwa kuondokewa na kiongozi wetu huyu, hatuna cha kusema zaidi ya kusema raha ya milele umpe bwana, na mwanga wa milele umwangazie, apumzike kwa amani,” asema Rais Samia.

Rais Samia akikagua gwaride maalum la kijeshi baada ya kuapishwa.
 

Rais Samia ametumia nafasi hiyo pia kuwashukuru viongozi wa Bunge na Mahakama kwa mshikamano walioonesha, lakini pia Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt Hussein Ali Mwinyi na mihimili yake kwa kuwa naye bega kwa bega katika kipindi hiki kigumu.

 

“Nawashukuru wenzangu katika Serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa ushirikiano katika kusimamia kipindi hiki cha mpito, Nawashukuru pia wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa ya amani na utulivu,

 

“Nawashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuliombea Taifa letu katika kipindi hiki kigumu, Kipekee nikishukuru chama changu - Chama Cha Mapinduzi kwa ukomavu wake na uongozi wake madhubuti ambao ndiyo msingi wa kuwezesha mabadiliko haya ya uongozi kwa amani na utulivu.

 

“Nitumie fursa hii pia kuwashukuru ndugu zetu wa vyama vya upinzania kwa salamu zao za kunitia nguvu, faraja na mshikamano walizokuwa wakinikikishia mara baada ya kutangaza msiba huu mkubwa.

 

“Katika mktadha huo huo, nawashukuru viongozi kutoka nchi jirani na nchi rafiki duniani kote waliotufikishia salamu za rambirambi kutokana na msiba huu mzito. Viilevile nivishukuru vyombo vyetu vyote vya habari ambao wamekuwa wakirusha mubashara matukio yote ya msiba huu, bila kuwasahau wasanii wetu ambao wametunga tungu na yimbo mbalimbali za faraja.

 

“Na mwisho japo sio kwa umuhimu, niishukuru familia yangu, hususan mume wangu, watoto wangu wapendwa, ndugu jamaa na marafiki, pamoja na ofisi ya Makamu wa Rais kwa kunitia nguvu na kunifariji katika nyakati hizi ngumu.

 

“Naahidi kuendelea kuwafariji na kuwashika mkono mjane wa Magufuli, familia yake na mama yake mzazi, Mungu awape moyo wa subira na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu. Natoa pia salamu za rambirambi kwa Watanzania wote kutokana pigo hili kubwa la msiba ambao hatukuutarajia,” amesema Rais Samia.

 

(Habari: Mara Online News)

Habari hii imechapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Sauti ya Mara, Machi 22, 2021.

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages