NEWS

Tuesday 16 March 2021

Wanufaika wa MWEA wawe chachu ya utunzaji mazingira bonde la mto Mara

Sehemu ya bonde la mto Mara upande wa wilaya ya Musoma
 

KUNA habari njema kwamba kikundi cha wanawake na vijana cha Nyanchabakenye kimeingizwa kwenye mpango wa kuwezeshwa mafunzo ya ujasiriamali yatakayowajengea uwezo wa kuendesha mradi wa kuweka na kukopa na mingine midogo midogo ya kujipatia kipato.

 

Kikundi hicho chenye wanawachama 28 kipo ndani ya bonde la mto Mara katika kijiji cha Nyanchabakenye, wilaya ya Rorya mkoani Mara. Ni miongoni mwa vikundi ambavyo ni wanachama wa Shirika lisilo la Serikali la MWEA (Mara Women Empowerment Assistance).

 

Hivi karibuni, wanachama wa kikundi hicho cha Nyanchabakenye walikutanishwa na viongozi wa Shirika la OIKOS lenye wataalamu wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali, jinsia na haki za binadamu.

 

Ushirikiano wa pande hizo unatarajiiwa kubadilisha maisha ya mamia ya wanachama wa MWEA katika vijiiji mbalimbali vilivyopo ndani ya bonde la mto Mara nchini Tanzania.

 

Vijiji hivyo ni Buswahili, Ketasakwa, Nyamerambaro, Kwibuse, Surubu na Mara Sibora.

 

Shirika la OIKOS lenye makao makuu yake jiijini Arusha, ndilo linatarajiwa kuwapa wanachama wa kikundi hicho mafunzo ya ujasiriamali, jinsia na haki za binadamu.

 

Hatua hiyo imetokana na juhudi za Shirika la MWEA ambalo limejikita katika kuwezesha wanawake na vijana kupitia mikopo midogo midogo ili kuwajengea uwezo wa kuondokana na maisha tegemezi.

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa OIKOS, Mary Birdi, shirika hilo limejikita pia katika kusaidia uboreshaji wa huduma ya maji na uhifadhi wa mazingira katika maeneo ambayo linaendesha shughuli zake.

 

Birdi anaongeza kuwa shirika hilo pia litawajengea wanachama hao wa MWEA uwezo Wa kuendesha miradi mbalimbali ya kijamii.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa MWEA, Mary Sange anasema mafunzo ya jinsia na haki za binadamu yatakayotolewa na OIKOS ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya shughuli za kijamii na kuchumi za wanachama hao.

 

Sange anaongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kupunguza nguvu ya mfumo mume na hivyo kuimarisha usalama wa mikopo ya wanachama wa MWEA.

 

Inaelezwa kwamba vikundi takriban 12 vitawezeshwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kimazingira na kiuchumi katika vijiji hivyo chini ya uratibu wa MWEA.

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa MWEA, Sange, miradi itakayoanzishwa ni pamoja na ufugaji kuku, uzalishaji vitalu vya miche ya miti ya aina tofauti, utengenezaji wa machujio ya maji, malambo ya maji na ufugaji nyuki.

 

Sange anasema kila kijiji/kikundi kimechagua mradi wake huku lengo kuu likiwa ni uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii kwa njia ya kipato.

 

Mkurugenzi huyo wa MWEA anasema hadi sasa shirika hilo limeshawafikia wanawake na viijana zaidi ya 10,000 katika wilaya za Musoma, Butiama, Bunda na Rorya tangu mwaka 2007 lilipoanzishwa.

 

Matarajio ya wengi sasa ni kwamba vikundi vyote ambavyo ni wanachama wa MWEA vitakuwa mfano na mabalozi wazuri wa kulinda na kutunza mazingira ya bonde la mto Mara unaomwaga maji yake katika Ziwa Victoria.

Muonekana wa sehemu ya bonde la mto Mara upande wa Tanzania.
 

Kama ambavyo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amekuwa akisisitiza, utunzaji wa mazingira ya bonde la mto Mara ni muhimu kwa amaendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa watu wanaishi ndani na hata nje ya bonde hilo.

 

Inaelezwa kwamba bonde hilo lina mchango mkubwa katika ustawi wa maisha ya watu zaidi ya milioni 1.1 katika nchi za Tanzania na Kenya.

 

Mazingira hai ya bonde hilo ni muhimu pia kwa ikolojia ya Serengeti na una mchango mkubwa katika uhifadhi wa wanyamapori ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo imetunukiwa Tuzo ya Hifadhi Bora Barani Afrika kwa miaka miwili mfululizo (2019 NA 2020).

Makundi ya nyumbu yakivuka mto Mara ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
 

Mkurugenzi wa Shirika la Wakulima na Wavuvi (VIFAFIO) Kanda ya Ziwa, Majura Maingu anasema mto Mara unasifika kimataifa kutokana na kuwezesha maisha ya wanyamapori katika hifadhi hiyo ambayo ni kivutio cha utalii cha kimataifa.

 

Afisa Uhusiano wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), Mhandisi Gerald Itimbula, anasema bonde la mto Mara lina umuhimu mkubwa kwa uhifadhi wa wanyamapori - akitolea mfano kitendo cha nyumbu ambao ni kuvutio kikubwa cha utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuuvuka mto huo kila mwaka.

 

Mto huo ambao unaanzia kwenye chemichemi za Enopuyapui katika misitu ya Mau nchini Kenya huchangia pia kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Kenya kupitia maadhimisho ya Siku ya Mara.

 

Kwa sababu hiyo, wanachama wa vikundi vyote vinavyowezeshwa na shirika la MWEA wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutunza bonde la mto Mara kwa kuepuka vitendo vya uharibifu na uchafuzi wa mazingira ya bonde hilo kwa manufaa ya jamii nzima.

 

(Imeandikwa na Christopher Gamaina wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages