
Na Christopher Gamaina
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 unakuja - ukiwa na umuhimu wa kipekee katika historia ya Taifa letu, Tanzania. Ni siku muhimu ya kufanya maamuzi kwa tathmini na matumaini mapya kwa mustakabali wa kizazi cha sasa na vijavyo.
Katika mazingira haya, kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura anayo nafasi ya kipekee na wajibu wa kikatiba wa kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia kwa amani na uzalendo.
Kupiga kura si kitendo cha kawaida tu cha kisiasa, bali ni kitendo cha kiungwana na la kizalendo. Ni njia halali na ya msingi ambayo wananchi huonesha ridhaa yao kwa viongozi wanaowaamini kuwa wataongoza kwa uadilifu, uwajibikaji na ufanisi.
Kura ni sauti ya raia, ni zana ya mabadiliko chanya, na ni msingi wa uhalali wa uongozi. Kujitokeza kwa wingi kupiga kura ni ishara ya uwajibikaji wa wananchi kwa taifa lao.
Kadiri Watanzania wengi watakavyoshiriki, ndivyo demokrasia yetu itakavyokuwa imara zaidi, ikionesha dunia kuwa Tanzania ni taifa lenye umoja na hekima katika kushughulikia mambo yake ya ndani kwa njia za kistaarabu.
Sheria za nchi na kanuni za uchaguzi zimewekwa ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, amani na uwazi. Ni wajibu wa kila mwananchi, chama cha siasa na taasisi kushiriki katika mchakato huu kwa kuzingatia misingi hiyo.
Kujihusisha na vitendo vya uchochezi, upotoshaji, vurugu au maneno ya kuwagawa Watanzania ni kinyume cha maadili ya taifa letu na ni kosa la kisheria.
Tofauti za kisiasa haziwezi kuwa sababu ya kuvunja umoja na mshikamano wetu. Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani, upendo na umoja - misingi ambayo kila mmoja wetu ana wajibu wa kuilinda.
Historia inaonesha wazi kwamba hakuna taifa linaloweza kustawi bila amani na utulivu. Uchaguzi ni tukio la muda mfupi, lakini madhara ya vurugu yanaweza kudumu kwa miaka mingi.
Kila Mtanzania anapaswa kuwa mlinzi wa amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Hili si jukumu la vyombo vya usalama pekee, bali ni wajibu wa kila raia kuzuia maneno, vitendo au mienendo inayoweza kuibua chuki na mgawanyiko.
Watanzania wote tuwe wazalendo wa kweli; tusikubali kutumiwa na mtu yeyote au kikundi chochote kuhatarisha amani ya taifa letu.
Vijana na wanawake ni nguzo muhimu ya taifa na nguvu kubwa ya mabadiliko. Asilimia kubwa ya wapiga kura nchini ni vijana; hivyo sauti yao ndiyo inayoamua mustakabali wa Tanzania. Ni muhimu kutumia nguvu hiyo kwa busara, kwa kujitokeza kupiga kura, si kwa kughafilika na propaganda au tamaa za muda mfupi.
Wanawake wana jukumu kubwa katika kusaidia kuhamasisha familia, jamii na majirani kujitokeza kupiga kura na kulinda amani.
Tanzania imebarikiwa kuwa na amani, uvumilivu wa kidini, kikabila na kisiasa. Huu ni urithi adimu unaopaswa kulindwa kwa hekima. Hivyo, uchaguzi ni fursa ya kuimarisha misingi hiyo, si kuivunja.
Tofauti za kisiasa ni jambo la kawaida katika demokrasia; kinachotutofautisha kama Watanzania ni namna tunavyoweza kuendesha tofauti hizo kwa busara na kuheshimiana.
Oktoba 29, 2025, Watanzania wote wenye sifa wanapaswa kujitokeza kwa wingi vituoni kupiga kura kwa amani na utulivu. Tufanye hivyo tukiwa na fahari kwamba tunatimiza wajibu wetu wa kikatiba, tunalinda amani ya taifa letu na tunajenga msingi wa maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na vijavyo.
Kura yako ni heshima yako, ni sauti yako, ni nguvu yako. Tuchague amani, tuchague umoja, tuchague maendeleo kwa Tanzania yetu, kwa vizazi vyetu. Tanzania Daima. Amani Kwanza. Umoja Kwanza. Maendeleo Kwanza.
No comments:
Post a Comment