NEWS

Friday 16 April 2021

Mbunge Chege, mfano wa kuigwa kwa utekelezaji ahadi

Mbunge wa Jimbo la Rorya mkoani Mara, Jafari Wambura Chege akichangia hoja Bungeni jijini Dodoma, hivi karibuni.

WAHENGA walisema dalili ya mvua ni mawingu na siku njema huonekana asubuhi. Maneno hayo sasa yanadhihirika wazi kwa Mbunge wa Jimbo la Rorya mkoani Mara, Jafari Wambura Chege.

 

Ikiwa ni takriban miezi minne imepita tangu wabunge wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waapishwe, Mbunge Chege ameweza kuwa- surprise wapigakura wake kwa mambo makubwa - ambayo mpaka sasa hayajaonekana kwa mbunge mwingine yeyote mkoani Mara.

 

Katika kipindi hicho kifupi, tayari mbunge huyu kijana ameshatekeleza ahadi kubwa kwenye sekta za afya, elimu, maji na barabara jimboni Rorya.

 

Ahadi alizotekeleza ni pamoja na uchangiaji wa gharama za ujenzi wa zahanati 17 katika vijiji vya Nyihara, Muhundwe, Kisumwa, Kenyamsana, Kigunga, Kukona, Oriyo, Manira, Nyanjage, Osiri, Roche, Deti, Mkoma, Nyabiwe, Ruhu, Makongro na Omunga.

 

Mbuge Chege ametumia fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kuchangia gharama za ujenzi wa zahanati hizo - ambapo ameunga mkono kila kijiji kwa wastani wa shilingi milioni tatu kugharimia ujenzi wa zahanati.

 

Pia, ameweza kununua gari la kubeba wagonjwa (ambulance), hivyo kuwaondolea wananchi wa Rorya mzigo waliokuwanao kwa muda mrefu wa kulazimika kulipa gharama kubwa kusafirisha mwili wa ndugu yao aliyefariki dunia.

Gari la kubeba wagonjwa (ambulance) ambalo Mbunge Chege amenunua na kulikabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wa jimbo hilo.
 

Kwa upande wa elimu, Mbunge huyo wa Rorya ameweza kumwomba Mkuu wa Wilaya kibali cha kuitisha harambee ya kuchangisha mabati kwa ajili ya kuezeka majengo ya shule za msingi na sekondari jimboni humo kwa lengo la kuwezesha wanafunzi kusoma bila msongamano madarasani.

 

Hadi sasa Mbunge Chege amefanikiwa kukusanya msaada wa mabati takriban 3,000 kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwamo wazaliwa wa Rorya na taasisi tofauti.

 

Katika sekta ya maji, tayari Mbunge Chege amewezesha uchimbaji wa visima virefu viwili katika vijiji vya Nyamasyeki na Mariwa na tayari wananchi wa maeneo hayo wameanza kunufaika na huduma ya maji safi.

Mtambo ukichimba kisima kirefu cha maji katika kijiji cha Nyamasyeki ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mbunge Chege.
 

Kwa upande mwingine, hivi karibuni mbunge huyo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ametekeleza ahadi kubwa ya kununua na kukabidhi katapila (grader) kwa wananchi wa Rorya - litakalotumika kulima barabara za kuunganisha vijiji na kata jimboni humo, hivyo kurahisisha shughuli za maendeleo zinazohitaji uwezeshaji wa miundombinu hiyo.

Mbunge Chege akikagua katapilla (grader) alilonunua na kuwakabidhi wananchi wa Rorya hivi karibuni kwa ajili ya kulima barabara za kuunganisha kata na vijiji jimboni humo.

Wananchi wa Rorya ni mashahi wa ahadi hizo zilizotekelezwa na Mbunge wao, Chege - ambaye pia ameonekana kufanya ziara za mara kwa mara katika kila kona ya jimbo hilo kuhamasisha shughuli za maendeleo ya kisekta.

 

Hakika Mbunge Chege amewadhihirishia wana-Rorya kuwa hawakukosea kumchagua, na wana kila sababu ya kujipongeza kwa kuchagua kiongozi sahihi, aliye tayari kushirikiana nao bega kwa bega katika kuinua hali ya maisha yao kijamii na kiuchumi.

 

Juhudi kubwa ambazo Mbunge Chege ameonesha katika kutatua kero za wananchi wa Rorya na kushughulikia maendeleo yao ya kisekta kwa vitendo, tena kwa muda mfupi wa siku 130 hivi tangu aanze rasmi majukumu ya kibunge, ni dalili tosha kuwa atakuwa mbunge wa mfano bora unaostahili kuigwa na wabunge wengine mkoani Mara kama si Tanzania kwa ujumla.

Kutoka kushoto ni Mbunge Chege, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga wakati waziri huyo alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maji wilayani humo, hivi karibuni.
 

Mbunge Chege amejidhihirisha kuwa ni kiongozi mchapakazi mahiri anayesimama kwenye ahadi zake. Anachohitaji zaidi ni ushirikiano wa dhati kutoka kwa wananchi na viongozi wengine katika jitihada za kuistawisha Rorya kimaendeleo.

 

Mwenyewe Mbunge Chege anaweka wazi kuwa shauku yake kubwa ni kuona uwajibikaji wake kwa wana-Rorya unaakisi kaulimbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan inayosema “Kazi Iendelee”, ili hatimaye aweze kuyafanya matatizo ya kijamii na kiuchumi jimboni Rorya kubaki historia.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

2 comments:

  1. Kweli kabisa, yeye ni chagio letu , Mungu amlinde na kumpigania azidi kufanya vizuri zaidi

    ReplyDelete

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages