NEWS

Monday 26 April 2021

Wanakijiji Karakatonga wapongezwa kutolisha mifugo hifadhini

Mhifadhi Thadeus Manonge kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (aliyesimama) akizungumza na wakazi wa kijiji cha Karakatonga, jana.
 

WANANCHI wa kijiji cha Karakatonga wilayani Tarime, Mara wamepongezwa kwa kutii sheria inayokataza watu kuingiza na kulisha mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

 

Pongezi hizo zimetolewa na Mhifadhi Thadeus Manonge kutoka kituo cha Ramai, wakati akizungumza katika kikao cha wahifadhi na viongozi wa Serikali ya Kijiji hicho, jana Aprili 26, 2021.

 

Kikao hicho ambacho pia kimewashirikisha maofisa wa idara za wanyamapori, ardhi na maliasili kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ni kwa ajili ya majadiliano ya kuboresha uhusiano na ujirani mwema kati ya Hifadhi hiyo na kijiji hicho.

 

“Mara ya mwisho kama sikosei ni mwezi wa 10, au wa 12 mwaka jana, mwaka huu [20201] leo ni mwezi wa nne ng’ombe hawajaingia hifadhini, tunawashukuru sana wananchi wa Karakatonga kwa hilo,” amesema Mhifadhi Manonge.

 

Mbali na ulishaji mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Diwani wa Kata ya Kwihancha kilipo kijiji hicho, Ragita Ragita amewataka wananchi hao pia kuachana na vitendo vingine vya ujangili ukiwemo uwindaji haramu wa wanyamapori katika hifadhi hiyo.

 

Aidha, Diwani Ragita amewataka maofisa watendaji wa vitongoji, vijiji na kata hiyo kuacha mazoea ya kuandika barua za kudhamini watuhumiwa wa ujangili wanaokamatwa akisema kitendo hicho kinakwaza juhudi za kukabiliana na uhalifu huo.

 

Wahifadhi kutokaa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kushirikiana na maofisa wa idara za wanyamapori, ardhi na maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wanaendelea na ziara ya kukutana na viongozi na wakazi wa vijiji 10 vilivyo jirani na hifadhi hiyo kujadiliana namna nzuri ya kushirikiana katika uhifadhi endelevu wa wanyamapori na mazingira.

 

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages