NEWS

Monday, 23 June 2025

Rais Samia aweka historia uzinduzi wa miradi mikubwa Mwanza, Simiyu



Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akisogeza kitambaa kuashiria uzinduzi wa Daraja la JP Magufuli “Kigongo–Busisi” lenye urefu wa kilomita tatu pamoja na barabara unganishi za kilomita 1.66 katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza wiki iliyopita. (Picha na Ikulu)
-------------------------------------------

Na Waandishi Wetu, Mwanza, Simiyu

Ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyotamatika juzi Jumamosi, imeacha alama na historia ya aina yake ya uzinduzi wa miradi mikubwa ya maendeleo katika mikoa ya Mwanza na Simiyu, ambayo inatarahiwa kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Kanda ya Ziwa.

Pamoja na miradi mingine, Rais Samia alizindua rasmi Daraja la kimkakati la JP Magufuli katika Ziwa Victoria linalounganisha maeneo ya Kigongo wilayani Misungwi na Busisi wilayani Sengerema, mkoani Mwanza.

Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilomita tatu na la kwanza kwa urefu Afrika Mashariki, umegharimu shilingi billion 718 kutokana fedha za ndani za kodi za wananchi.

“Lengo limetimia. Daraja hili litakuwa alama kwa nchi yetu… ni fahari nyingine kubwa kwa nchi yetu. Tunauona mwanga wa dhana ya kujitegemea,” alisema Rais Samia na kueleza faraja yake kuzindua daraja hilo.

Aidha, Rais Samia alizindua Mradi wa Maji Butimba wenye thamani ya shilingi bilioni 71.6, utakaosambaza maji safi kwa wakazi takriban 450,000 wa jiji la Mwanza na viunga vyake.

Kwa upande mwingine, mkuu huyo wa nchi alifungua Jengo la Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Simiyu lililopo mjini Bariadi, kisha akazindua Shule ya Sekondari ya Wasichana ya mkoa huo iliyogharimu shilingi bilioni 4.4.

Shule hiyo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuwekeza na kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa kike katika mikoa ya pembezoni, kwa lengo la kuongeza ufaulu, kupunguza vikwazo vya kijinsia katika elimu, na kuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Pia, Rais Samia aliweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Shule ya Amali Mwamapalala katika wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, kwa niaba ya shule nyingine 26 za aina hiyo zinazojengwa Tanzania Bara, kwa lengo la kuwezesha wahitimu kuwa na uwezo wa kujitegemea na kuendana na mahitaji ya ajira.

Vilevile, Rais Samia alizindua Mradi wa Maji Lamadi wenye thamani ya shilingi bilioni 12.83, kisha kuweka jiwe la msingi la mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wenye thamani ya shilingi bilioni 440 utakaonufaisha wananchi wa wilaya zote za mkoa wa Simiyu, yaani Busega, Itilima, Bariadi, Maswa na Meatu.

Katika ziara hiyo, Rais Samia aliambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa, akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira na mawaziri wa wizara mbalimbali, miongoni mwa wengine.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages