Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Hamis Mkaruka Kura akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo asubuhi |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime kimetangaza kuwasimamisha wenyeviti wa mitaa kadhaa kutoendelea na wadhifa huo kwa madai ya kufanya uasi.
Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Hamis Mkaruka Kura ametoa tamko
hilo kupitia mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake, leo Aprili 28, 2021.
Mkaruka amesema waliosimamishwa ni wenyeviti wa mitaa walioshiriki
mkutano ulioitwa "umoja wa wenyeviti wa mitaa mji wa Tarime"
uliofanyika jana kwenye ukumbi wa hoteli moja mjini Tarime na kudai kuwa
hawako tayari kufanya kazi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias
Ntiruhungwa.
Katibu huyo amesisitiza kuwa waliohusika katika mkutano huo
wameasi taratibu za chama hicho.
“Wale wote waliosikika wakizungumza kwenye vyombo vya habari
kuanzia leo (Aprili 28, 2021) tunawasimamisha uenyeviti mpaka hapo
tutakapowaita kwenye vikao vya maadili na vikao vingine kutoa maamuzi
mengineyo,” amesema Mkaruka.
Amesema Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime kinaridhshwa na
utendaji kazi wa Mkurugenzi huyo wa Mji wa Tarime na kwamba kama kuna wenyeviti
wana jambo dhidi yake walipaswa kufuata utaratibu.
“Huyo Mkurugenzi sisi katusadia sana, anafanya vizuri kazi za
umma,” amesisitiza Mkaruka.
Ameongeza kuwa mkutano huo umekiuka taratibu za chama hicho tawala
huku akikishutumu kikundi cha wafanyabiashara ambacho amedai kiko nyuma ya
sakata hilo kwa maslahi binasfi ambayo yanawezea kufifisha utendaji na ufanisi
katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
“Kwanza hatuna kitu kinaitwa umoja wa wenyeviti wa mitaa kisheria
na hatuna mwenyekiti wa umoja wa wenyeviti, huo ni uasi,“ amesema Katibu huyo
wa CCM.
Mkaruka amesema vikao vyote vinavyojadili maslahi ya Chama
vinafanyika ndani ya ukumbi wa CCM Wilaya, hivyo chama hicho kinaamini
kilichofanywa na wenyeviti hao sio sahihi.
“Na ukumbi wamekodi na wakanywa na soda, ni nani aliwafadhili, na
tuna ukumbi wa kutosha watu 600 na hakuna mtu aliomba akanyimwa, tafasiri yake
tunajua kuna watu wako nyuma yao ambao ni waasi wenzao na tunaendelea kutafuta
mmoja mmoja,(akimanisha waliowezesha mkutano huo kufanyika),” amesema
Mkaruka bila kuweka wazi idadi wa wenyeviti wa mitaa waliosimamishwa wadhfa
wao.
Katika hatua nyingine, Katibu huyo wa CCM Wilaya ameomba mamlaka
husika kutatua mgogoro wa vibanda vya wafanyabiashara katika mji huo
badala ya kuingia katika mabishano.
“Chama Cha Mapinduzi tunatoa agizo leo, ndani ya siku saba tupate
majibu, tofauti na hapo tutachukua hatua kwa kila mhusika,“ ametahadharisha
Mkaruka.
(Habari na picha: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment