NEWS

Thursday 27 May 2021

Benki ya CRDB yatoa milioni 5/- kupiga jeki uzinduzi wa Muongozo wa Uwekezaji Mkoani MaraMkuu wa mkoa wa Mara, Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi (katikati), Katibu Tawala wa Mkoa huo, Caroline Mtapula (kushoto) na Meneja Biashara wa CRDB Kanda ya Ziwa, Hassanaly Japhary wakati wa makabidhiano ya hundi ya Sh milioni tano mjini Musoma, leo.


BENKI ya CRDB imetoa hundi yenye thamani ya Shilingi milioni tano kwa ajili ya kusaidia kufanikisha shughuli ya uzinduzi wa Muongozo wa Uwekezaji Mkoani Mara, utafanyika mjini Musoma kesho Ijumaa.

Akikabidhi hundi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi mjini Musoma leo Mei 27, 2021, Meneja Biashara wa CRDB Kanda ya Ziwa, Hassanaly Japhary amesema benki hiyo imetoa msaada huo kuunga mkono juhudi za Serikali ya mkoa wa Mara katika kuboresha mazingira ya uwekezaji mkoani humo.

Japhary amesema Benki ya CRDB iko tayari kufanya kazi bega kwa bega na Serikali ya mkoa wa Mara kwa lengo la kuleta maendeleo kwa manufaa ya wakazi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Ameongeza kuwa mbali na hundi hiyo, benki hiyo pia imetoa fulani 100 kwa ajili ya tukio la uzinduzi huo ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.


Meneja Biashara huyo amesema msaada uliotolewa na CRDB ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa kurudisha fadhila kwa wananchi na wateja wao, huku akiwataka wananchi kuunga mkono jitihada za benki hiyo kwa kutumia huduma zao.

 
Akipokea hundi hiyo, RC Gabriel mbali na kuishukuru Benki ya CRDB kwa msaada huo, ametoa wito kwa wadau mbalilmbali kuiga mfano huo ili kuleta maendeleo endelevu mkoani Mara.
 

RC Gabriel amesema Muongozo wa Uwekezaji utakaozinduliwa kesho ni nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Mara wenye fursa nyingi za uwekezaji ambazo zikitumika vizuri zitasaidia katika ukuaji wa uchumi.
 

Amesema Serikali mkoani Mara imeamua kutumia fursa hizo kuleta mapinduzi ya kiuchumi ili kuwanufaisha wakazi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

MaraOnlineNews-Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages