NEWS

Monday 3 May 2021

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria yawashirikisha wazee utunzaji vyanzo vya maji

Wazee wa mila kutoka vijiji mbambali wilayani Tarime wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) mara baada ya kukutana katika kikao cha kuweka mikakati ya kuhifadhi vyanzo vya maji ikiwemo visima vya asili, hivi karibuni.


BODI ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imekutana na wazee wa mila wilayani Tarime, Mara kuweka mikakati ya pamoja ya kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji vya asili.

 

Kikao hicho kimeandaliwa na LVBWB kupitia ofisi zake za Dakio la Mara-Mori zilizopo Musoma mkoani Mara, hivi karibuni.

 

“Mkutano huu ni utekelezaji wa sera na sheria katika kuwashirikisha wadau wote kushiriki kutunza vyanzo vya maji wakiwemo wazee ambao kihistoria wamekuwa watunzaji wazuri wa vyanzo vya maji pamoja na milima,” Afisa Maji wa Dakio la Mara-Mori, Mhandisi Mwita Mataro amewambiwa waandishi wa habari katika eneo la mkutano huo.

 

Mhandisi Mataro amesema kikao hicho ni cha kwanza kuandaliwa na LVBWB na kuhusisha wazee wa mila kuweka mikakati ya kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji.

 

Ameongeza kuwa ushirikishwaji wa wazee wa mila katika kutunza vyanzo vya maji ni muhimu kwani ni kundi lenye maamuzi na linaloheshimika katika jamii.

 

“Wazee wa mila wana sauti katika jamii na wamekuwa na mbinu zao za kulinda vyanzo vya maji kama visima vya asili ambavyo vipo mpaka leo, hivyo tumeona ni muhimu tukutane nao,” Mhandisi Mataro ameiambia Mara Online News mara baada ya mkutano huo uliofayika katika eneo la Nyamwaga, kilometa chache kutoka mto Tigithe na Mgodi wa dhahabu wa North Mara.

 

Wazee hao wametaja shughuli zinazotishia uhai wa vyanzo vya maji kuwa ni kilimo kando kando ya vyanzo vya maji, upandaji wa miti isiyo rafiki wa mazingira na uchimbaji ovyo wa madini jirani na vyanzo vya maji.

Kikao cha wazee wa mila kutoka vijiji mbambali vya wilaya ya Tarime na watendaji wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji kikiendelea eneo la Nyamwaga, hivi karibuni.

 

Baada ya kupata elimu katika kikao hicho, wazee hao wamesema wataungana na Serikali katika kulinda na kuhifadhi vya vya maji.

 

“Elimu hii ya Bonde [LVBWB] imetufanya kugundua kuwa maji ni kitu muhimu sana kwa viumbe vyote na sisi kama wazee tuna sehemu yetu katika jamii, mfano  kutunza miti ya asili ambayo ina mchango mkubwa katika kuleta mvua,” amesema Simon Magachi, mmoja wa washiriki wa kikao hicho kutoka kata ya Nyamwaga.

 

Magachi amesema kuanzia sasa watawataka wananchi kuondoa miti yote isiyo rafiki katika vyanzo vya maji na kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa vyanzo vya maji.

 

“Kwa kuwa ofisi ya Bonde imeamua kuleta miti tutaondoa miti yote isiyo rafiki na kupanda ambayo ni rafiki mazingira,” amesema Magachi ambaye ni kiongozi wa jamii katika kijiji hicho.

 

Wazee hao wameomba kushirikishwa katika kusimamia uendelevu wa vyanzo vya maji kwa kushirkiana na serikali za vijiji na jumuiya za watumia maji.

 

Pia, wameiomba LVBWB kuharakisha shughuli ya kupima ubora wa vyanzo vya maji katika maeneo ya dakio la Mara-Mori kwa usalama wa afya za watumiaji.

 

Baadhi ya maazimio ya kikao hicho ni pamoja na kuweka mpango wa pamoja ambao utakuwa endelevu katika kutunza vyanzo vya maji. Suala la kutenga maeneo ya marisho na kilimo pia lilijadiliwa katika kikao hicho.

 

Wadau wengine waliohudhuria kikao hicho ni wenyeviti wa vijiji vinane kutoka maeneo ya mto Tigithe na maeneo jirani, Mamlaka ya Usambazaji Maji Vijijini na Mijini (RUWASA), Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na baadhi ya walimu kutoka shule jirani.

 

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages