NEWS

Saturday 15 May 2021

Changamoto za kilimo mseto katika bonde la mto Mara



Kilimo mseto kinaendeshwa kiholela katika bonde la mto Mara kutokana na wakulima husika kutokuwa na elimu ya kanuni bora za kilimo hicho

KILIMO mseto ni mfumo wa kukuza mimea, au mazao ya aina tofauti katika shamba moja; mfano mahindi na alizeti, mtama na ulezi, migomba na kahawa, mchicha na bamia, n.k.

Manufaa ya mfumo wa kilimo mseto ni pamoja na kuzalisha mazao ya aina tofauti katika eneo dogo, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuimarisha rutuba ya ardhi.

Hata hivyo, pamoja na faida hizo, wakulima wa kilimo mseto katika bonde la mto Mara nchini Tanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazokwaza uzalishaji wenye tija.

Tatu Steven ni mmoja wa wakulima wanaoendesha kilimo mseto katika kijiji cha Kwisaro kilichopo ndani ya bonde la mto Mara wilayani Butiama, anataja mojawapo ya vikwazo wanavyokabiliana navyo kuwa ni ukosefu wa elimu ya kanuni bora za kilimo hicho.

“Hatuna elimu ya kitaalamu kuhusu kilimo mseto, tunalima tu kiholela,” anasema Tatu katika mahojiano maalumu na Mara Online News kijijini Kwisaro, hivi karibuni.

Tatu ambaye pia ni Katibu wa Kikundi cha Umoja VICOBA cha kuweka na kukopeshana fedha - chenye wananchama 27, anataja baadhi ya mazao wanayolima kuwa ni mahindi, mtama, ufuta na karanga.

Mkulima mwingine katika kijiji hicho, Thomas Marwa anaungana na Tatu kusisitiza kuwa ukosefu wa mbinu bora ni kikwazo kikubwa cha ufanisi wa kilimo mseto katika eneo hilo.

“Kila mtu huku kijijini anajilimia shamba lake kiholela, tunapanda mbegu kwa kurusha, mtu unalima shamba kubwa unavuna kidogo,” anasema Marwa.

Wakulima hao wanasema kilimo wanachofanya ni cha kujikimu tu kwani sehemu kubwa ya mazao wanayozalisha ni kwa ajili ya chakula na sehemu ndogo tu ndio wanauza kwa ajili ya kupata fedha za kununua mahitaji mengine ya kifamilia.

“Tuna ardhi kubwa kwa ajili ya kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara, tukipata elimu au mafunzo ya kilimo bora tutaweza kuongeza uzalishaji,” anasema mkazi mwingine wa Kwisaro, Mairi Magabe.

Magabe anasema uzalishaji wa mazao kama ufuta na karanga ukiongezeka utashawishi wafanyabiashara wakubwa kujitokeza kuwekeza katika viwanda vya kukamua mafuta ya mazao hayo na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi na kuboresha hali ya maisha ya wakulima kijijini hapo.



Patrick Maregeri akivuna nyanya kwenye shamba lake katika bonde la mto Mara wilayani Butiama

Mhandisi Gerald Itimbula ambaye ni Ofisa Uhusiano wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) linalojumuisha bonde la Mto Mara, anasema elimu ya kanuni bora za kilimo mseto kwa wakulima itasaidia pia kupunguza uchafuzi wa vyanzo vya maji katika bonde hilo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalam, Profesa Rwekaza Mukandala amewahi kunukuliwa katika mkutano wa wadau wa kilimo akisema kilimo mseto kina tija kutokana na mkulima kutumia eneo dogo kulima mazao ya aina mbili hadi tatu tofauti.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Kilimo Tanzania (www.kilimo.go.tz), Serikali inao mkakati wa kutoa elimu kwa maofisa ugani wote nchini ili nao waweze kuelimisha wakulima kanuni bora za kilimo mseto, hasa maeneo ya vijijini.

Kutoka kulia ni Mairi Magabe, Tatu Steven na Thomas Marwa, wakazi na wakulima wa kijijini Kwisaro wakati wa mahojiano na Mara Online News kijijini hapo, juzi.
 
Msamba Chacha ambaye ni Ofisa Mhamasishaji kutoka Shirika la MWEA linawezesha vikundi vya kijamii kuondokana na maisha duni, anasema shirika hilo lina taarifa za uhitaji wa mafunzo ya kanuni bora za kilimo mseto kwa wakazi wa Kwisaro.

“Tuna taarifa ya ukosefu wa elimu ya kanuni bora za kilimo kikiwemo cha mseto kwa wakazi wa kijiji cha Kwisaro na maeneo mengine ya bonde la mto Mara,” anasema Chacha na kuendelea:

“Kwa kuwa moja ya majukumu yetu kama Shirika ni kuwaunganisha wanavijiji na wataalamu husika, tunajipanga kupeleka wataalamu wa kilimo kuwajengea wakazi wa Kwisaro uwezo wa kuendesha kilimo kwa kutumia kanuni bora na za kisasa.” 

(Habari na picha: Christopher Gmaina wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages