NEWS

Friday 14 May 2021

Wachimbaji wadogo Mara kupatiwa mafunzo ya uchukuaji bora wa sampuli za uchunguzi na uchenjuaji madini kuanzia kesho Jumamosi



Wachimbaji wadogo wa madini wakiwa kazini mkoani Mara

WIZARA ya Madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeandaa mafunzo ya siku tatu kwa wachimbaji wadogo wa madini mkoani Mara kuhusu namna bora ya uchukuaji wa sampuli za uchunguzi na uchenjuaji wa madini.

Akizungumza na Mara Online News mjini Musoma leo, Mjiolojia Mwandamizi kutoka GST na Mratibu wa Mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo Taifa, John Kalimenze amesema mafunzo hayo yataanza kesho Jumamosi Mei 15 hadi Jumatatu Mei 17, 2021.

Kalimenze amefafanua kuwa mafunzo ya kesho yatafanyika mjini Musoma kwa nadharia na siku mbili zinazofuata yatakuwa ya vitendo katika maeneo ya Buhemba, Nyamongo, Ikungu na Gedeli.


Kalimenze akizungumza na Mara Online News mjini Musoma leo

“Mafunzo haya ni mwendelezo wa mkakati wa Wizara ya Madini wa kusaidia wachimbaji wadogo nchi nzima na hapa Mara katika kanda hii ya Ziwa ni sehemu yetu ya mwisho ya mafunzo haya ya awamu ya kwanza, ambapo tumeanza na mikoa tisa,” amesema Kalimenze na kutaja mikoa hiyo kuwa ni Dodoma, Singida, Tanga, Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Geita, Shinyanga na Mara.

Ameongeza “Mafunzo haya yamewalenga hasa wachimbaji wadogo katika mkoa huu wa Mara kuwasaidia namna bora ya kuchukua sampuli za uchunguzi na uchenjuaji wa madini.

“Tunajua kabisa bila kuchukua sampuli vizuri hakuna uzalishaji wenye tija, kwa hiyo tunategemea sasa mafunzo haya yatawajengea wachimbaji wadogo uwezo, kwanza kufanya tafiti makini na wenye tija kwa kuchukua sampuli sahihi na kuzipeleka maabara kwa ajili ya kujua kama zina madini wanayoyataka.

“Pili, katika uchenjuaji tunakwenda kuwafundisha namna bora ya kuchukua sampuli za uchenjuaji, kuzipima kujua tabia ya marudio, wayachunguze marudio yao ili wajue ukiachana na dhahabu, marudio yao yanaambatana na madini gani mengine ili waweze kuchenjua kwa tija.

“Sisi kama Serikali tunategemea kwamba wachimbaji wadogo mkoa wa Mara watabadilika na kunufaika katika uzalishaji wa madini na hatimaye kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na pato la Taifa kwa ujumla.”


Ukosefu wa teknolojia ya kisasa ni moja ya matatizo yanayowakabili wachimbaji wadogo wa madini mkoani Mara

Kalimenze ametoa wito kwa wachimbaji wadogo wa;liopo mkoani Mara kuhudhuria kwa wingi mafunzo hayo kwenye ukumbi wa uwekezaji uliopo ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mara mjini Musoma,kesho.

Ofisi za Soko Kuu za Dhahabu Mkoa wa  Mara lililopo mjini Musoma

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages