NEWS

Wednesday 12 May 2021

DC Msafiri awapa Waislamu futari



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri (wa pili kulia) akishiriki swala pamoja na viongozi wa Kiislamu katika Msikiti wa Ijumaa mjini Tarime, juzi.

VIONGOZI wa dini wameombwa kuongeza kasi ya kuhubiri amani ili kubadilisha tabia za watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu katika jamii.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Mtemi Msafiri katika Msikiti wa Ijumaa mjini Tarime, juzi Mei 10, 2021 wakati wa kula futari aliyoiandaa kwa ajili ya waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi wengine.


Mhandisi Msafiri (wa nne kushoto) na wenyeji wake wakipata futari.

Mhandisi Msafiri ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa jamii kushirikiana katika kutafuta ufumbuzi wa ongezeko la watoto wa mitaani katika mji wa Tarime ili kuepusha matatizo makubwa katika siku zijazo.

“Hawa watoto wa mtaani wana wazazi, kwa hiyo ni vyema kila mzazi akachukua jukumu lake kuhakikisha wanakuwa katika mazingira bora, kuwaacha mtaani hili ni bomu la baadaye Tarime, ardhi yetu inakubali kila kitu, niwaombe tulime, tupendane, tuthaminiane wana-Tarime,” amesema Mkuu huyo wa wilaya.


Mhandisi Msafiri (katikati) na masheikh kadhaa msikitini

Akizungumza katika swala hiyo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amewataka waumini wa dini ya Kisilamu kushikamana na kuthamini waumini wa madhehebu mengine ili kudumisha upendo na amani nchini.

Nao baadhi ya viongozi wa madhehebu ya Kikristo na Kiislamu wamempongeza Mkuu wa Wilaya, Mhandisi Msafiri, kwa hatua ya kuwakutanisha katika futari hiyo wakisema kitendo hicho kimeacha alama kubwa kwao, huku wakiahidi kuendeleza umoja na upendo bila kujali tofauti za madhehebu yao.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages