NEWS

Friday 21 May 2021

Mara Online yakabidhi msaada wa vitabu Tarime SekondariOFISA Mtendaji Mkuu (CEO) wa Mara Online News, Jacob Mugini amekabidhi msaada wa vitabu mbalimbali vya kiada na ziada vya wanafunzi wa kidato cha tano na sita vyenye thamani ya Shilingi milioni 5.2 katika Shule ya Sekondari ya Tarime mkoani Mara.

Msaada huo umetolewa chini ya ufadhili wa mdau wa maendeleo, Nyambari Nyangwine kupitia kwa Mugini ambaye ndiye aliyemwomba vitabu hivyo kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo.


CEO wa Mara Online, Jacob Mugini (wa pili kulia) akikabidhi msaada wa vitabu kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tarime, Mwalimu Machota Edward Kora. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Mwalimu Laurent Chacha na kulia ni Mhariri Mkuu wa Mara Online News na Gazeti la Sauti ya Mara, Christopher Gamaina.

Mugini ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Blogu ya Mara Online News na Gazeti la Sauti ya Mara, amekabidhi vitabu hivyo kwa Bodi, walimu na wanafunzi wa shule hiyo, jana Mei 21, 2021.

“Sisi kama Mara Online tunaunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua kiwango cha taaluma kwa wanafunzi wetu. Baada ya Serikali kutumia mamilioni ya fedha kukarabati shule hii tumeona ni vizuri tulete msaada huu wa vitabu.

“Ninamshukuru Mungu na nimefurahi sana kutimiza ahadi ya msaada wa vitabu hivi kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi katika masomo na ninatumaini shule hii itakuwa rafiki wetu wa karibu,” amesema Mugini ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.Makabidhiano ya vitabu yakiendelea. Wa kwanza kushoto ni mke wa CEO, Rhoda Mugini.

Mugini amemshukuru Nyangwine kwa kufadhili upatikanaji wa vitabu hivyo ndani ya muda mfupi baada ya kuombwa msaada huo.

"Namshukuru sana Nyambari Nyngwine kwa kuendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo ya elimu nchini na ameniambia niwambie anawapenda sana na kwamba siku akija Tarime atafika shuleni hapa kuwasalimia," amesema.

Hadi sasa, Nyangwine ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mwaka 2010 hadi 2015, ameshatoa msaada wa vitabu vyenye thamani ya Shilingi bilioni mbili kwa ajili ya wanafunzi wa shule mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani (Zanzibar)


Makabidhiano ya msaada wa vitabu yamekamilika sasa.

Katika hafla ya makabidhiano ya vitabu hivyo, Mugini amefuatana pia na wafanyakazi wengine wa taasisi ya Mara Online, Winnie Magaria, Emmanue Daniel na Yohana Gitano.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tarime, Mwalimu Machota Edward Kora amewashukuru Mugini na Nyangwine akisema wamepata silaha itakayowawezesha kufanya vizuri zaidi katika masomo na kuwatakia kila la heri wadau hao wa maendeleo.

“Sisi kama shule kwa kweli tumepata furaha kubwa sana, umetupa msaada mkubwa sana ambao hata mahafali ambazo tulikuwa tukifanya hatukuwahi kupata msaada wa namna hii, Mungu ameendelea kujidhihirisha… Zawadi hii si ndogo, maarifa yanapatikana kwa kusoma.

“Umetupatia silaha, sisi tunakuahidi kuingia vitani, sisi tuko tayari kupambana, sisi tuko tayari kukuletea ushindi na sisi tuko tayari kukupa heshima. Mungu wa mbinguni akubariki, abariki kazi ya mikono yako, ambariki mfadhili wako, aibariki familia yako na aibariki taasisi yako,” amesema Mwalimu Kora.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo ya wavulana, Mwalimu Laurent Chacha naye amewashukuru Mugini na Nyangwine kwa msaada huo akisema wameweka alama ya aina yake shuleni hapo.

“Hamna kitu cha maana kama elimu, mtu anayekushawishi usome ni rafiki yako kwa sababu utafanikiwa hapo mbeleni. Kwa kweli umetenda kitu kitakachoacha historia hapa shuleni. Sisi tukuombee tu kwa Mungu, najua neno asante ni dogo sana lakini kwa niaba ya Bodi nasema asante sana, asante sana,” amesema Mwenyeki huyo wa Bodi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Mwalimu Chacha (aliyesimama) akitoa neno la shukurani baada ya mapokezi ya msaada wa vitabu hivyo.

Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Lucas Chacha ameshukuru akisema “Mungu awaweke kwenye nafasi kubwa mfanye makubwa zaidi.”

Huku Mwalimnu Edson Japhet akisema “Umetupa matumaini makubwa, Mungu aendelee kuwabariki na utufikishie salamu kwa huyo mfadhili, mwambie tumefurahi sana na tumepokea msaada huu kwa mikono miwili.”

Nao wanafunzi wa shule hiyo, Praise Ayub, John Chacha na Emmanuel William wameshukuru wakisema vitabu hivyo vitawaongezea ari ya kusoma zaidi na kuahidi kutimiza lengo la shule hiyo la kuwa miongoni mwa shule 10 bora kitaifa katika mhithani wa kuhitimu kidato cha sita mwakani.


Baadhi ya wanafunzi wa Sekondari ya Tarime walioshiriki hafla ya makabidhiano ya msaada wa vitabu hivyo.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya msaada huo wa vitabu ni pamoja na Kaimu Afisa Elimu Wilaya ya Tarime, Mwalimu Magreth Mwema, Afisa Elimu Kata ya Bomani, Mwalimu Thabitha Kesowani na Mwenyekiti wa CCM wa Kata hiyo, Maulid Juma.

Wanafunzi wa shule ya sekondari Nkende ya mjini Tarime wakiwa na moja laptop iliyotolewa na Mara Online

Taasisi ya Mara Online inamiliki chombo cha habari cha kidigitali (Mara Online News) na Gazeti pekee la kanda ya Ziwa la Sauti ya Mara ambalo limezidi kupata wasomaji wengi hadi vijijini .

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime Elias Ntiruhungwa akipokea msaada wa saruji kutoka kwa mwakilishi wa Mara Online 
CEO wa Mara Online amekuwa akitoa misaada ya kijamii huku akitoa umuhimu katika sekta ya elimu .


(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages