NEWS

Monday 10 May 2021

Tuboreshe kilimo cha mbogamboga, matunda kwa maendeleo ya watuZao la kabichi

KILIMO cha mbogamboga na matunda (horticulture) kinaweza kuleta mabadiliko ya maisha ya watu kwa kutoa ajira, kuboresha afya zao, kuhamasisha uwekezaji na kuongeza pato la taifa iwapo juhudi madhubuti zitafanyika kukiwezesha kuwa cha kisasa zaidi.

Aidha, kipaumbele kiwe kuwapa motisha wakulima kwa kutoa elimu ya kilimo cha kisasa, vitendea kazi na hata ujenzi wa ‘greenhouse’ na kuwatafutia masoko nje ya nchi.

Nchini Tanzania, hususan mkoani Mara, kilimo cha mbogamboga na matunda hujumuisha mazao ya bustani kamvile nyanya, kabichi, spinachi, sukumawiki, bamia, tikiti maji, papai, matango na mengineyo.

Haya ni mazao yanayohitaji umakini mkubwa katika uzalishaji, kuanzia utayarishaji wa shamba, mbegu, matumizi ya viuatilifu, mbolea, uvunaji, uhifadhi na masoko.

Wilayani Rorya, Mara wakulima wadogo wamechangamkia biashara hii kwani wanasema licha ya changamoto mbalimbali, hiki ni kilimo cha muda mfupi na soko lake hupatikana kwa haraka, wakati mwingine hapo hapo shambani.

Kwa mujibu wa Siproza Charles Nyadhi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumiaji Maji Mara Kaskazini inayojumisha vijiji vinane wilayani Rorya, wakulima wanazalisha nyanya na kabichi kwa ajili ya kujikimu.

“Tunalima nyanya na kabichi. Tulijaribu tikiti maji lakini mvua zikawa nyingi kwa hiyo tukaacha,” amesema Siproza na kuongeza kuwa licha ya shamba la jumuiya, kila mwanakikundi anakuwa na shamba lake binafsi.

Siproza Charles akionesha shamba la mbogamboga lililopo eneo oevu katika bonde la mto Mara

Hata hivyo, Siproza anakiri kwamba hakuna takwimu zinazoonesha pato la kila mwezi kwani uzalishaji unategemea mwenendo wa soko.

“Kama soko limefurika nyanya kwa mfano, inabidi wakulima wauze kwa bei yoyote ile kuepuka hasara ya kuharibikiwa mao.

Kukosekana kwa takwimu za mapato na mlolongo mzima wa kilimo hiki, kunadhihirisha uwepo wa pengo kubwa katika ufuatiliaji wa kukua ama kudumaa kwa sekta hii ndogo lakini muhimu katika sekta nzima ya kilimo.

Naye Scolastica Julius, anasema kilimo cha mbogamboga ni mkombozi wa mkulima, japo kina changamoto lukuki.

"Nimeweza kujenga nyumba ya vyumba viwili na watoto wangu watatu wanapata mahitaji yao ya msingi," anasema mama huyo mjane.

Daniel Charles anakizungumzia kilimo cha mbogamboga kama mtaji wa biashara. "Nilianza na matuta manne, sasa hivi nina nusu ekari ya nyanya na kabichi. Nimeajiri vijana wawili na nimefungua duka la vyakula," anasema.

Kuhusu changamoto za kilimo hiki, wakulima wanasema ni vigumu kusonga mbele kwa hali ilivyo sasa.

"Tunahitaji wafadhili, lakini la muhimu ni kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa. Hatuna ujuzi wa kujua ubora wa mbegu, matumizi ya mbolea na viuatilifu. Tunatumia uzoefu wetu kutambua vipimo vinavyostahili. Pia hatuna soko la uhakika. Tunauza tu kwa wapita njia na wachuuzi wadogo wadogo," anasema Siproza.

Tungependa kuona mageuzi katika kilimo cha mbogamboga na matunda, kwani kinaendeshwa na wakulima wengi wadogo ambao wanahitaji mafunzo na uwezeshwaji ili waachane na uzalishaji wa mazoea na kuufanya uwe wa tija.

Wakulima hawa wakiachwa peke yao, ni dhahiri kuwa nchi inapoteza mapato mengi.

Kwa mujibu wa taasisi ya TAHA, asilimia 70 ya kilimo cha mbogamboga na matunda kinaendeshwa na wakulima wadogo.

Ripoti ya utafiti ya TAHA ya mwaka 2015, TAHA inasema kilimo hiki kinachangia asilimia 38 ya pato la kigeni linalotokana na kilimo.

TAHA ni taasisi kubwa inayojishughulisha na kilimo cha mbogamboga na matunda nchini Tanzania.


Zao la tikiti maji

Kuna kila sababu ya wadau husika kufuatilia na kutatua changamoto zinazowakabili wakulima wa mazao haya.

Mapema mwaka huu, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Andrew Masawe alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kipaumbele ni kuona wizara inapeleka teknolojia ya kisasa kwenye uzalishaji wa mazao ya wakulima, ikiwemo utatuzi wa kero zao.

Tunatarajia kuona teknolojia ikitumika katika kilimo cha mbogamboga na matunda, ikiwemo utaalamu wa ‘greenhouse’ kuwezesha wakulima kuzalisha mazao yao muda wote wa mwaka, iwe masika au kiangazi.

Ni wazi kwamba uzalishaji utaongezeka kwa kiwango kikubwa na hii itazaa fursa ya kuuza bidhaa zetu nje ya nchi.

Vilevile, kuongezeka kwa mbogamboga na matunda yenye viwango kutavutia wawekezaji katika sekta ya viwanda. Hii ni katika kukidhi dhima ya mlolongo wa thamani, kuongeza ajira na pato la taifa.

(Uchambuzi: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages