NEWS

Sunday, 23 November 2025

AICT, Right to Play wajenga kesho bora ya watoto wa kike Tarime, Serengeti



Baadhi ya wanafunzi wa kike wa Shule ya Msingi Itiryo wilayani Tarime wakifurahia picha ya pamoja, huku wakionesha zawadi za jezi za michezo zilizotolewa na AICT na Right to Play wakati wa tamacha la uhamasishaji jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike wiki iliyopita

Na Joseph Maunya
Akiripoti kutoka
Tarime, Serengeti
-----------------------

Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe na Shirika la Kimataifa la Right to Play wametajwa kama wajenzi wa kesho bora kwa watoto wa kike wanaoishi katika wilaya za Tarime na Serengeti, mkoani Mara - kwa kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kutoa elimu kwa kundi hilo.

Hayo yalisemwa na wanafunzi na wazazi mbalimbali waliohudhuria tamasha la michezo la uhamasishaji jamii juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike – lililofanyika chini ya ufadhili wa taasisi hizo katika viwanja vya Shule ya Msingi Itiryo wilayani Tarime, wiki iliyopita.

"Hawa wageni wetu (AICT, Right to Play) wamekuwa msaada mkubwa sana kwa mabinti kwa sababu wanawasaidia kupata elimu kwa ajili ya kesho yao bora, tofauti na sisi ambao leo tunataabika kutokana na kukosa elimu," alisema Nyamosi Chacha Mwita, mkazi wa kijiji cha Itiryo.


Baadhi ya wazazi waliohudhuria tamasha la uhamasishaji jamii juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike.

"Mimi nawashauri wazazi wengine wasiwaozeshe wasichana wenzetu, wawalete shuleni wasome ili kesho na keshokutwa tupate wanawake wengine ambao ni mashupavu kama Rais wetu mama Samia," alisema Getrude Peter, mwanafunzi wa darasa la sita.

Awali, tamasha lingine la uhamasishaji jamii la AICT na Right to Play lilifanyika wilayani Serengeti katika kata ya Stendi Kuu na kujumuisha wanafunzi kutoka shule za msingi Kambarage A na Kambarage B, ambapo washiriki walipongeza juhudi za taasisi hizo katika kumkomboa mtoto wa kike kupitia elimu.

Kwa upande wake Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo, alisema AICT na Right to Play wanashirikiana kupitia mradi wa "Save Her Seat" katika wilaya za Tarime na Serengeti, ili kusaidia watoto wa kike kupata haki zao na kufikia malengo yao.


Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo, akielezea mradi wa 'Save Her Seat'.

"Sisi kama AICT tumekuwa tukishirikiana na Right to Play, na lengo letu ni kuhakikisha kwamba watoto wa kike wanasaidiwa kwa kila namna ili wamalize masomo yao na kufikia ndoto zao waweze kunufaika na elimu katika siku za usoni," alisema Fungo.

Kwa mujibu wa Fungo, mradi huo wa "Save Her Seat" ulianza mwaka 2023 ambapo mbali na kutoa elimu, pia taasisi hizo zinatoa zawadi za vinywaji na vifaa vya michezo kwa wanafunzi wa shule husika.


Wanafunzi wa Shule ya Msingi Itiryo wakipokea zawadi za jezi za michezo zilizotolewa na AICT na Right to Play.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages