NEWS

Thursday 13 May 2021

Ufugaji nyuki kwa maendeleo na uhifadhi wa mazingira



Nyuki

UFUGAJI nyuki kibiashara vijijini ni shughuli inayokua kwa haraka, hasa kwa sababu inahamasisha ushirikiano na ubunifu na pia inaenda sambamba na uhifadhi mazingira.

Tangu kale, walikuwepo wafugaji nyuki wakitumia zana duni kutundika mzinga mmoja au miwili, na zaidi sana asali haikuwa biashara. Ilitumika tu kama dawa au mbadala wa sukari kwenye chai.

Aidha, katika maeneo mengine nchini, wafugaji nyuki waliharibu mazingira kwa kuchoma moto msituni wakati wa usiku, ambao ndio muda pekee waliweza kurina asali.

Lakini kadri miaka inavyokwenda, kumekuwa na mageuzi makubwa katika ufugaji nyuki na watu wanaelewa faida ya kufuga kibiashara na kutunza mazingira. Uvunaji unafanyika mchana kweupe kwa sababu mfugaji anazo zana za kumkinga asing'atwe na nyuki.

Ikumbukwe kuwa nyuki wanahitaji mazingira safi na yenye utulivu ili waweze kutengeneza asali. Manzuki (shamba la uzalishaji) ni mandhari ya kuvutia kwani lazima iwe na miti ya maua, maji, kivuli na kusiwe na kero kama vile kelele za watu, wadudu, mfano sisimizi au hata nyoka.

Hili ni jambo la kutia moyo kwani ni kama kuua ndege wawili kwa jiwe moja.

Akizungumzia ufugaji wa nyuki kibiashara, Gabriel mkazi wa wilayani Tarime anasema mbali na kutafuta kipato, kitu kingine kilichomsukuma kuingia kwenye ufugaji nyuki ni kutokana na kukithiri kwa uharibifu wa mazingira. Gabriel ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wafugaji Nyuki Tarime, anasema awali kulikuwa na ukataji miti kiholela kwa ajili ya kuchoma mkaa.

Pia wakulima walichoma moto mashamba ovyo. Hata hivyo aliweza kuwashawishi wakabadilika na kuunda mtandao wao.

"Huwezi kutenganisha ufugaji nyuki na uhifadhi mazingira. Ni kama Kulwa na Doto," anasema Gabriel.




Mkulima akionesha mzinga wa ufugaji wa kisasa wa nyuki

Naye Lameck Nyasagati, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji ya Tobora, wilayani Serengeti anakiri kwamba ufugaji nyuki na uhifadhi mazingira vinakwenda pamoja.

Jumuiya yake ambayo ina vijiji 22 na mamlaka ya mji mdogo wa Mugumu, iliweza kushawishi wachoma mkaa 19 kuacha shughuli hiyo na kujiunga na ufugaji nyuki kibiashara.

"Tuna mizinga 160 na tunafuga nyuki kwenye maeneo ya hifadhi ya serikali. Faida ni kubwa kwa sababu tunangojea tu kuvuna. Hatuna tatizo la kutafuta mtaji wa kuwekeza. Ni shughuli endelevu maana huwezi kuweka mizinga nyuki wakakosa kuingia," anasema Lameck.

Umuhimu wa kuwa na vikundi vya uzalishaji unajidhihirisha wakati wa kutafuta mafunzo, kubadilishana mbinu mbalimbali jinsi ya kutatua changamoto na upatikanaji wa masoko.

Kwa kulitambua hilo, Gabriel alihamasisha kuundwa kwa ushirikiano wa wafuga nyuki Tarime

"Lengo letu kubwa lilikuwa ni kuwa na sauti ya pamoja katika kutatua matatizo. Tunataka tuanzishe kituo cha ukusanyaji asali (collection centre) ambacho ni kama mnada utakaotoa bei elekezi. Tutaweka pia takwimu za mapato ili tujue kwa mwaka tunazalisha kiasi gani na mwenendo wa biashara yetu. Tuko mbioni kuanzisha kanzi data na kujiwekea malengo," anaeleza Gabriel.




Baadhi ya wafugaji nyuki wakifuatilia mafunzo ya mbinu za kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao ya nyuki kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Tarime.

Umoja huu ambao kwa hakika ni nguvu, umewapa hamasa pia wanawake. Ufugaji nyuki sio tena kazi ya wanaume pekee kama ilivyokuwa hapo zamani. Wapo wanawake wafugaji binafsi, pia vipo vikundi vitatu vya kina mama.

Ushirikishwaji wa kina mama kwenye jumuiya na mitandao mbalimbali ya uzalishaji kunasaidia kuondoa mfumo dume na dhana potofu kwamba wanawake hawana uwezo wa kufanya shughuli fulani fulani.

Mafunzo pia yamesaidia kuimarisha ufugaji nyuki kibiashara. Haya ni muhimu katika dhana nzima ya mnyororo wa thamani.

Ukiuza asali kwenye chupa ya maji iliyotumika, chupa ya pombe, ndoo au dumu la maji, wateja hawatakuwa na imani na wewe. Watatilia shaka utayarishaji wako. Lakini kama utauza adali kwenye kifungashio chenye jina la kampuni yako na namba za simu, ule mwonekano tu wa kifungashio unatosha kumvutia mteja.

Kanuni Kanuni ambaye ni Afisa Miradi wa WWF ofisi ya Mara anasema kati ya mambo ambayo shirika lake limesaidia wafugaji nyuki ni pamoja na kuwafundisha mbinu mbalimbali za kuvutia masoko, ili kuifanya iwe shughuli endelevu.

"Tunaangalia mpango biashara wao ili kujua nini kinaingia nini kinatoka na kuwapa maelekezo ya mlolongo mzima wa thamani," anasema Kanuni na kuongeza kuwa hii ni pamoja na kuwataka kutumia mikutano na kwenda kwenye mahoteli makubwa kuuza bidhaa zao.

Watoa mafunzo wengine ni Wakala wa Misitu (TFS) ambao pamoja na mambo mengine wamewaasa wafugaji kuanzisha chama cha ushirika ili kuwa na soko la pamoja. Akiendesha mafunzo ya siku moja ambayo yalijumuisha wafugaji 100 kutoka vikundi 50 vya wilaya za Tarime, Musoma, Bunda na Serengeti, Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Tarime, Charles Agustin Masawe alisema, "Ufugaji nyuki unasaidia uhifadhi mazingira na kutunza misitu.

Naye Mary Makang'a kiongozi wa kikundi cha wafugaji cha Ikoma Cultural Centre, alisema amejifunza kuchakata asali na kuongeza thamani mazao ya nyuki,pia kutengeneza vifungashio bora.



Ni Dhahiri kwamba hakuna shughuli yoyote ya uzalishaji isiyokuwa na changamoto. Kilio kikubwa cha wafugaji nyuki ni soko la uhakika.

Lakini soko haliwezi kumfuata mkulima, sharti alitafute, Kama alivyosema Kanuni.

Leo hii mitandao ya kijamii inatumika katika kutangaza biashara. Ni muhimu kwenda na wakati. Bidhaa za nyuki zinahitajika kote duniani. La msingi ni kufuata kanuni na masharti ya uandaaji kuanzia kwenye manzuki hadi ufungashaji. Ni shughuli yenye tija na endelevu.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages