
Diwani Mteule wa Kata ya Matongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Godfrey Kegoye (CCM).
Tarime
-----------
Diwani Mteule wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye (CCM), amechukua fomu kuwania nafasi ya Uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), hatua ambayo inaonekana kuvuta hisia za wengi kutokana na rekodi yake ya utendaji.
“Nimechukua fomu jana na leo Ijumaa nairudisha katika ofisi zetu za CCM Wilaya,” Kegoye ameiambia Mara Online News leo asubuhi, akionesha kujiamini na utayari wa kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Kegoye, maarafu kama ‘God’, alichaguliwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 kuongoza tena kata ya Matongo kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Anasema endapo atapata ridhaa ya chama chake, atashirikiana kikamilifu na madiwani wenzake, viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo kuanzisha zama mpya za mageuzi ya maendeleo ya kisekta ndani ya halmashauri hiyo.
“Lengo langu kubwa ni kuwatumikia na kuwaletea wananchi wa Tarime Vijijini maendeleo bila ubaguzi wowote, sitabagua kijiji wala kata, maendeleo yataenda kila kona ya halmashauri yetu. Nitasimamia vizuri mapato ya hamashauri - kila senti itumike vizuri kwa maendeleo ya wananchi wetu,” amesisitiza.
Kegoye ambaye anatajwa kama kiongozi mahiri, mnyenyekevu, mchapa kazi na asiye na makundi au siasa chafu, amesema Tarime Vijiini inastahili kuwa moja ya maeneo yenye kasi kubwa ya maendeleo kama ‘Singapore’.
Anabainisha kuwa halmashauri hiyo imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali kama vile madini, wanyamapori na ardhi inayostawisha mazao mbalimbali, ikiwemo kahawa aina ya Arabia inayotamba katika soko la dunia.
Kata yake ya Matongo, inaripotiwa kuwa miongoni mwa kata zilizofanikiwa kutekeleza miradi ya mifano kwenye sekta mbalimbali, zikiwemo afya na maji katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
No comments:
Post a Comment