NEWS

Monday 24 May 2021

Wananchi bonde la mto Mara wapelekewe elimu ya kanuni bora za kilimo msetoSehemu ya bonde la mto Mara wilayani Butiama, Tanzania.

KILIMO mseto ni mfumo wa kupanda na kuzalisha mazao ya chakula na biashara ya aina tofauti katika shamba au eneo moja.

Faida za kilimo hicho ni pamoja na kumwezesha mkulima kupata chakula na fedha kwa ajili ya matumizi mengine ya kifamilia.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalam - Tanzania, Profesa Rwekaza Mukandala amewahi kunukuliwa katika mkutano wa wadau wa kilimo akisema kilimo mseto kina tija kutokana na mkulima kutumia eneo dogo kulima mazao ya aina mbili hadi tatu tofauti.

Faida nyingine za kilimo mseto ni kuimarisha rutuba ya ardhi, kuzuia mmomonyoko wa udongo, kutoa ajira kwa wananchi wengi na kuchangia pato la Taifa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Kilimo Tanzania (www.kilimo.go.tz), sekta ya kilimo kikiwemo cha mseto ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Taarifa za wizara hiyo zinaonesha kuwa hadi mwaka 2017, sekta ya kilimo ilikuwa inatoa ajira kwa asilimia 65.5 na kuchangia asilimia 29.1 ya pato la Taifa, asilimia 30 ya soko la nje na asilimia 65 ya malighafi za viwanda.

Wakazi wengi wa bonde la mto Mara nchini Tanzania wanategemea kilimo mseto kwa ajili ya kuendeleza maisha kijamii na kiuchumi. Wanalima mazao ya chakula yakiwemo mahindi, mhogo na mtama pamoja na mazao ya biashara kama vile matikiti maji, pamba na alizeti.

Hata hivyo, wakulima hao wanakabiliwa na ukosefu wa elimu ya kanuni bora za kilimo mseto.


Elimu ya kanuni bora ya kilimo mseto kama hiki inahitajika kwa wananchi wa bonde la mto Mara.

Mmoja wa wakulima katika kijiji cha Kwisaro kilichopo ndani ya bonde la mto Mara wilayani Butiama, Tatu Steven anathibitisha ukosefu wa elimu hiyo.

“Hatuna elimu ya kitaalamu kuhusu kilimo mseto, tunalima tu kiholela,” anasema Tatu katika mahojiano maalum na Mara Online News kijijini Kwisaro, hivi karibuni.

Anaja baadhi ya mazao wanayolimwa kwa wingi kijijini hapo kuwa ni pamoja na mahindi, mtama, ufuta na karanga.


Mtama na mahindi ni miongoni mwa mazao yanayolimwa katika bonde la mto Mara.

Hakuna shaka kwamba tatizo la ukosefu wa elimu ya kanuni bora za kilimo mseto linalowakabili wakulima katika kijiji cha Kwisaro ndiyo hali halisi kwenye vijiji vingine ndani ya bonde la mto Mara.

Hivyo kuna haja ya mamlaka husika kuchukua hatua ya kupeleka elimu hiyo kwa wakulima wanaoendesha kilimo mseto katika bonde hilo ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa ajili ya kuboresha hali za maisha yao kijamii na kiuchumi.

Ni wazi kuwa ufumbuzi wa tatizo hilo linalowakabili wakulima wanaoishi katika bonde la mto Mara uko mikononi mwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo.

Kilimo mseto kinachozingatia kanuni bora kitakuwa na tija kwa wananchi wanaoishi katika bonde la mto Mara.

Wadau kama vile Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) na Shirika la MWEA waone umuhimu wa kujitokeza kupeleka elimu ya kanuni bora za kilimo mseto kwa wakulima hao ili kuwajengea maarifa ya kuendesha kilimo cha mazao ya chakula na biashara kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

“Tuna ardhi kubwa kwa ajili ya kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara, tukipata elimu au mafunzo ya kilimo bora tutaweza kuongeza uzalishaji,” anasema mkazi mwingine wa Kwisaro, Mairi Magabe.

Magabe anaongeza kuwa uzalishaji wa mazao kama ufuta na karanga ukiongezeka utashawishi wafanyabiashara wakubwa kujitokeza kuwekeza katika viwanda vya kukamua mafuta ya mazao hayo na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi na kuboresha hali ya maisha ya wakulima kijijini hapo.

Mhandisi Gerald Itimbula ni Ofisa Uhusiano wa LVBWB inayojumuisha bonde la mto Mara. Anakiri kwamba elimu ya kanuni bora za kilimo mseto kwa wakulima itasaidia pia kupunguza uchafuzi wa vyanzo vya maji katika bonde la mto huo unaomwaga maji katika Ziwa Victoria ambalo mtambao wake unaunganisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

(Imeandikwa na Christopher Gamaina)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages