NEWS

Tuesday 1 June 2021

Mpango wa matumizi bora ya ardhi hauna mbadala bonde la mto MaraWakazi wa bonde la mto Mara wanategemea shughuli za kilimo, ufugaji na uchimbaji madini kama inavyoonekana katika eneo hili la Nyamongo wilayani Tarime.

MPANGO wa matumizi bora ya ardhi ni mpangilio au utengaji wa ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile makazi, kilimo, miundombinu, malisho ya mifugo, hifadhi ya misitu, huduma za kijamii na kiuchumi. Ni mpango wenye faida nyingi za kijamii, kiuchumi na kimazingira.

Hata hivyo, bado mpango huu haujaanzishwa katika vijiji vingi vilivyopo ndani ya bonde la mto Mara unaomwaga maji katika Ziwa Victoria nchini Tanzania.

Bonde hili lina ukubwa wa kilomita za mraba 13,325 na wananchi wasiopungua 1,100,000 wanaotegemea shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi na uchimbaji madini kuendesha maisha yao.

Wananchi wanaoishi katika bonde la mto Mara hawajaweza kunufaika ipasavyo na bonde hili kutokana, kikwazo kinaweza kuwa ni ukosefu wa mpango wa matumizi bora ya ardhi.


Mifugo ikiwa kwenye malisho jirani na mto Mara wilayani Butiama

Mkazi wa kijiji cha Kewanja, wilaya ya Tarime mkoani Mara, Lameck Mang’era anasema amekuwa akisikia mpango wa matumizi bora ya ardhi ukizungumzwa tu kinadharia na baadhi ya viongozi kwenye vyombo vya habari, lakini haujapewa msukumo kijijini hapo.

“Kwa jinsi ambavyo nimekuwa nikisikia watu wakiuelezea mpango huo redioni, ninapata picha kwamba ukianzishwa katika kijiji chetu tutapata maendeleo makubwa,” anasema Mang’era katika mazungumzo na Mara Online News, hivi karibuni.

Shauku hiyo ya Mang’era, inawakilisha wananchi wengi kutuma ujumbe kwa Serikali na wadau wa maendeleo na uhifadhi wa mazingira, kuongeza msukumo wa kuhamasisha na kuwezesha uanzishaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kila kijiji ndani ya bonde hili.

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Tanzania, ni miongoni mwa wadau wanaoweza kuhamasisha na kusaidia uanzishaji wa mpango huo katika vijiji hivyo.

Majukumu ya Tume hiyo yaliyoainishwa kwenye tovuti yake (www.nlupc.go.tz) ni pamoja na kuzijengea mamlaka za chini (zikiwemo za vijiji) uwezo wa kupanga, kutekeleza na kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi.


Mkulima akivuna nyanya shambani katika bonde la mto Mara wilayani Butiama.

Pia, NLUPC kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inatekeleza programu zinazolenga kuimarisha uelewa wa jamii katika upangaji, utekelezaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi.

Zaidi ya hapo, Tume hiyo ina jukumu la kuanzisha na kuimarisha programu za elimu juu ya umuhimu na ushiriki katika usimamizi wa rasilimali ardhi.

Afisa Ardhi na Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Rhoida Nyondo anasema faida za mpango wa matumizi bora ya ardhi ni pamoja na kuepusha migogoro ikiwemo ya kugombea matumizi na mipaka ya ardhi, mfano kati ya kijiji na kijiji.

“Mpango huu unawezesha wananchi wakiwemo wanawake kunufaika na ardhi yao baada ya kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali kulingana na mahitaji yao,” anasema Rhoida.


Rhoida akielezea umuhimu wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika mkutano na viongozi wa kijiji cha Masurura wilayani Tarime. Kijiji hicho ni miongoni mwa vingi ambavyo havijaanzisha mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Rhoida anaongeza “Mfano, kuainisha na kutenga maeneo ya huduma za jamii kama vile zahanati, shule, maji na barabara, lakini pia shughuli za kilimo, malisho ya mifugo, hifadhi ya misitu, n.k.”

Kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi, kundi la wanawake huweza kunufaika zaidi kutokana na kusogezewa karibu huduma za maji na afya.

Aidha, mpango wa matumizi bora ya ardhi ni moja ya vigezo muhimu vinavyowezesha wananchi kupimiwa ardhi yao na kupewa hati miliki, ambazo wanaweza kuzitumia kuweka dhamana ili kukopeshwa mitaji ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi.

“Kwa kuwa sheria ya umiliki wa ardhi nchini kwetu [Tanzania] haina ubaguzi wa kijinsia, mpango wa matumizi bora ya ardhi unampatia hata mwanamke haki ya kumiliki ardhi na kuitumia katika kujiinua kiuchumi,” anasema Rhoida.

Mbali na kusaidia kuboresha hali ya maisha ya wananchi kijamii na kiuchumi, na uendelevu wa mto Mara, mpango wa matumizi bora ya ardhi katika bonde hili utasaidia pia kulinda ikolojia ya Serengeti ambayo ni muhimu kwa uhifadhi wa wanyamapori, mazingira na shughuli za utalii.


Makundi ya nyumbu wakivuka mto Mara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

Kwa ujumla, mpango wa matumizi bora ya ardhi hauna mbadala kwa wakazi wa bonde la mto Mara. Ukosefu wa mpango huu ni kikwazo cha maendeleo ya wananchi katika bonde hili.

Hivyo, mamlaka za kiserikali na wadau mbalimbali sasa waone umuhimu wa kuunganisha nguvu za kuwezesha uanzishaji wa mpango huu ili kuharakisha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira katika bonde hilo.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages